Majaliwa awasili kuaga waliofariki ajali ya ndege Bukoba

Majeneza yenye miili ya watu 19 waliofariki katika ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Jumapili Novemba 6, 2022 ikiwa imebeba watu 43 kutumbukia katika Ziwa Victoria, Bukoba mkoani Kagera.
Muktasari:
- Waziri mkuu Kassimu Majaliwa pamoja na viongozi wengine wa kitaifa wamewasili uwanja wa Kaitaba kwa ajili ya kuaga miili ya watu 19 waliofariki jana kwenye ajali ya ndege ya Precision Air.
Bukoba. Waziri mkuu Kassimu Majaliwa pamoja na viongozi wengine wa kitaifa wamewasili uwanja wa Kaitaba kwa ajili ya kuaga miili ya watu 19 waliofariki jana kwenye ajali ya ndege ya Precision Air.
Ajali hiyo imehusisha ndege aina ya ATR 42-500 ilikuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Bukoba na ilipotaka kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba iliangukia ziwani, mita 100 kutoka ulipo uwanja wa ndege.
Katika ajali hiyo, Watu 19 walifariki dunia huku wengine 26 wakiokolewa katika jitihada zilizofanywa na wananchi wa Bukoba wengi wao wakiwa wavuvi katika Ziwa Victoria pamoja na vyombo vingine vya uokoaji.
Miili ya watu hao inaagwa leo Jumatatu Novemba 7, 2022 katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kabla ya miili hiyo kukabidhiwa kwa ndugu.
Majaliwa amefika katika uwanja huo muda mfupi baada ya miili 19 kuwasili katika uwanja huo.
Viongozi wengine waliowasili ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, mkuu wa Operseheni wa Jeshi la Polisi nchini, Juma Awadhi, wakuu wa mikoa mbalimbali na viongozi wengine.