Majaliwa azindua mwongozo kukomesha rushwa ya ngono vyuoni

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

  •  Waziri mkuu, Kassim Majaliwa leo Alhamisi Novemba 25,2021 amezindua mwongozo wa uanzishwaji wa madawati ya jinsia kwenye vyuo vikuu na vya kati.



Dar es Salaam. Waziri mkuu, Kassim Majaliwa leo Alhamisi Novemba 25, 2021 amezindua mwongozo wa uanzishwaji wa madawati ya jinsia kwenye vyuo vikuu na vya kati.

Mwongozo huo unalenga kukomesha vitendo vya rushwa ya ngono vinavyoelezwa kushamiri kwenye taasisi za elimu ya juu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, Majaliwa amesema nguvu kubwa inatakiwa kuongezwa katika kukabiliana na tatizo hilo linaloathiri vijana wengi wa kike.

Majaliwa amesema vita dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia inapaswa kushirikisha watu wote wanaochukia vitendo hivyo.

Amebainisha  hatua  ya kuanzishwa kwa mwongozo inaweza kuwa mwarobaini wa kumaliza tatizo hilo la unyanyasaji kwa mabinti waliopo vyuoni.

Ameeleza  taasisi za elimu ya juu  ni maeneo ambayo mara kadhaa Serikali  imekuwa ikipata  taarifa za uwepo wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

“Tunahitaji Watanzania kuthamini maisha ya kila mmoja wetu, tunataka kila Mtanzania awe huru, anayesoma asome kwa uhuru."

“Ninaendelea kusisitiza uanzishwaji wa madawati ya jinsia kwenye vyuo vyote. Hii ni ajenda na ilani ya CCM nasisitiza haki na usawa na kuwalinda Watanzania dhidi ya ukatili wa kijinsia," amesema akitumia fursa hiyo kuwataka wadau wa masuala ya jinsia kutumia siku 16 kujadili upungufu  wa sheria ili ziboreshwe.

“Maboresha haya yakiletwa yatafanyiwa kazi kwa haraka yakifika bungeni, tunataka Watanzania wote waishi kwa matumaini makubwa."