Majaliwa: Bado kuna ufinyu wanawake viongozi
Muktasari:
- Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema bado kumekua na changamoto ya ufinyu wa wanawake kwenye nafasi za juu za uongozi, hivyo wanapaswa kuelimishwa zaidi kwa maana haitoshi kuwachagua, kuwateua na kuwapa nyadhifa wanawake watumishi kama hawajaelimika vya kutosha.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema suala la usawa wa kijinsia ni muhimu kwenye kufikia maendeleo endelevu, hivyo wanawake wanahitajika zaidi katika nafasi za juu za uongozi.
Amesema bado kumekua na changamoto ya ufinyu wa Wanawake kwenye nafasi za juu za uongozi.
Hayo yamesemwa leo Mei 5, 2023 na Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene wakati akisoma hotuba ya Waziri Mkuu kwenye mahafali ya programu za uongozi zinazotolewa na Taasisi ya Uongozi.
"Nimefarijika sana, kufahamu kuna programu maalum ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake, maana haitoshi kuwachagua, kuwateua na kuwapa nyadhifa wanawake watumishi kama hawajaelimika vya kutosha.
"Juhudi za kukwamua wanawake lazima ziendane na juhudi za kulea na kukuza vipaji vyao vya uongozi ili wanapopatiwa nafasi waweze kuonyesha kwa vitendo namna gani wanawake wanaweza kubadili jamii na kuleta maendeleo," amesema
Amewaasa viongozi wanawake wanaohitimu mafunzo hayo wakaonyeshe kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kufanya maamuzi kwa kujiamini na zaidi wakashirikane na akina baba katika utendaji.
"Wanawake, kuwezeshwa kielimu na kiuchumi isiwe sababu ya kuibua jeuri na majivuno mara mpandapo vyeo au kuongezeka kwa pato lenu, mkifanya hivi mtaharibu juhudi za Serikali.
"Lengo letu ni kuwa na viongozi wanawake watakaokuwa chachu ya kuleta maendeleo kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa. Tunaamini Wanawake walioelimika ni chachu ya maendeleo yenye tija kwa jamii nzima," amesema Majaliwa.
atika hatua nyingine, amesema moja ya changamoto kuu ni gharama za uendeshaji mafunzo hayo inayosababisha taasisi ya uongozi kuanzisha mfumo wa uchangiaji gharama.
Amesema uchangiaji wa gharama ni muhimu sana ili kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu hivyo amewasihi viongozi wa Wizara, Idara na Taasisi nyingine za umma na binafsi kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo hayo ili viongozi na watumishi waweze kujiunga.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema ili kiongozi afanikiwe lazima mifumo ifanye kazi hivyo wanaendelea kuboresha mifumo.
"Ili kiongozi akue lazima asome vitabu na machapisho mbalimbali, viongozi wengi hawapati muda wa kujiendeleza lakini sisi tunatoa poa mafunzo ya mtandaoni, nawahimiza wanawake viongozi kuchangamkia fursa hii."