Majaliwa: Magufuli ameacha alama nchi nzima
Muktasari:
- Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Hayati John Magufuli ameacha alama kwa kila Mtanzania kutokana na utendaji wake uliotukuka.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Hayati John Magufuli ameacha alama kwa kila Mtanzania kutokana na utendaji wake uliotukuka.
Majaliwa ameeleza hayo leo Jumatano Machi 24, 2021 wakati wa kuaga mwili wa kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.
“Mwanza ni mahali pa kihistoria kwa kiongozi wetu ambaye tunamuaga leo, ameishi, amefanya kazi, amejenga mahusiano na watu mbalimbali na hata katika utumishi wake amefanya mambo makubwa yanayoweka alama hapa kanda ya ziwa.”
“Kiongozi wetu wameiacha alama Taifa zima kila mahali mpaka vijijini na ndiyo sababu leo Watanzania kila mahali wanalia kwa uchungu kwa kuondokewa na jemedari wao,” amesema Majaliwa.
Akitoa salamu za pole kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Majaliwa amesema ameagizwa kuwasihi wananchi katika kipindi hiki cha huzuni cha kuondokewa na mpendwa wao kuwa watulivu.
“Anawaomba sana kwanza tuwe watulivu na kuendelea kufanya shughuli zetu tukiwa na utulivu tushikamane, kushirikiana, kupendana kama ilivyokuwa hapo awali.”
“Rais Samia anayo matumaini kwamba katika kipindi hiki si tu mpaka Machi 26 (siku ya maziko) bali siku zote 21 za maombolezi tutakuwa watulivu kila mmoja kwa dini yake na dhehebu lake tuendelee kumwombea ili Mungu amuweke mahali salama,” amesema Majaliwa.