Majaliwa: Wazazi wapunguzieni watoto majukumu wapate muda wa kusoma

Majaliwa: Wazazi wapunguzieni watoto majukumu wapate muda wa kusoma

Muktasari:

  • Waziri mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi kuhakikisha  wanawapunguzia watoto majukumu ya  nyumbani ili  kuwawezesha kupata muda wa kujisomea na kupumzika.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi kuhakikisha  wanawapunguzia watoto majukumu ya  nyumbani ili  kuwawezesha kupata muda wa kujisomea na kupumzika.

Majaliwa amesema hayo leo Jumanne Februari 23, 2021 wakati akizungumza na walimu, wanafunzi na wazazi baada ya kukagua miundombinu ya shule ya msingi Mitope, Ruangwa mkoani Lindi.

Amesema iwapo watoto watapata muda mzuri wa kujisomea na kupumzika itawasaidia  kuwaongezea ufaulu kwenye masomo yao na kutimiza ndoto zao.

Mbali na hilo, Majaliwa  amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wananunuliwa vifaa vyote vinavyohitajika shuleni  zikiwemo  sare, madaftari sanjari na kufuatilia mienendo yao kielimu.

”Wazazi tufuatilie na kujiridhisha kama watoto wetu wanafika shule na kuingia madarasani. Pia tuwe tunakagua madaftari yao na pale tunapoona hawafanyi vizuri tuwasiliane na walimu,” amesema Majaliwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa amesema atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake kuendelea kusimamia vizuri shughuli za maendeleo.

Mgandilwa ameahidi kuendelea kusimamia vyema  fedha zote za maendeleo zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya Wilaya hiyo ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mwalimu Mkuu wa shule  hiyo,  Margareth Mselewa amesema  walimu wamejipanga vizuri kuhakikisha wanafunzi wote wa darasa la saba wanafaulu kwa asilimia 99.