Majambazi wateka magari matatu na kupora Mbarali

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa  Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mbarali na Mkuu wa Wilaya Kanali Denis Mwila ,  tukio hilo limetokea usiku wa  Aprili 26,2023 katika mlima Mwami Kata  ya  Mswisi  barabara kuu ya Tanzania na nchi Jirani ya Zambia(Tanzam).

Mbeya. Watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi  wakiwa na silaha za jadi wameteka magari matatu eneo la mlima Mwami Kata  ya Mswisi wilayani Mbarali katika barabara kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam) usiku wa kuamkia leo Aprili 26,2023.

 Akizungumza na Mwananchi digital leo Jumatano Aprili 26,2023 Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Mwila amethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba limetokea saa 8.30 usiku.

“Majambazi hao baada ya kufanikiwa kusimamisha magari hayo walifanya uharibifu kwenye vioo vya mbele kwenye magari mawili likiwepo basi la abiria ambayo yote yalikuwa yakitokea Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenda Jijini Dar es Salaam.”amesema

Ameongeza kuwa “Baada ya kufanya uharibifu huo ndipo waliokwenda kwenye gari ndogo lililokuwa likisafirishwa (IT) na kupora dola za Marekani 200 (Sh430,000) na fedha za kitanzania 150,000 (jumla Sh580,000)”

Kanali Mwila amesema taarifa za awali zimebaini gari lililotumiwa na majambazi hao ni aina ya Toyota Noah ambayo inaendelea kufuatiliwa ili kubaini watu waliohusika na tukio hilo.

”Tunashukuru Mungu hakuna mtu aliyepata madhara kutokana na tukio hilo kwa sasa tumeliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua zaidi sambamba na kuona ya kuimarisha usalama kwa mabasi na magari ya masafa marefu,”amesema.

Mkazi wa Mswisi ,Jane Joel ameliambia Mwananchi kwa simu kuwa eneo hilo ni hatari sana nyakati za usiku na kuomba Serikali kuweka utaratibu wa kusindikiza mabasi na magari madogo yanayofanya safari za usiku.