Majaribio uzalishaji umeme Bwawa la Nyerere yaanza rasmi

Muktasari:

  • Taarifa hiyo kwa umma imetolewa Desemba Mosi, 2023; Tanesco imefafanua kuwa kazi hiyo inahusisha kuunganisha kituo cha umeme cha Chalinze kitakachopokea umeme kutoka JNHPP na gridi ya taifa.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kazi ya kuunganisha Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) na gridi ya Taifa imeanza kwa majaribio.

Taarifa hiyo kwa umma imetolewa Desemba Mosi, 2023; Tanesco imefafanua kuwa kazi hiyo inahusisha kuunganisha kituo cha umeme cha Chalinze kitakachopokea umeme kutoka JNHPP na gridi ya taifa.

"Kazi hii itakapokamilika itawezesha kupeleka umeme wa gridi kwenye mitambo ya umeme ya Bwawa la Nyerere (JNHPP) kwa ajili ya kuanza majaribio ya mitambo hiyo," imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Tanesco, kuanza kwa zoezi hilo ni mafanikio makubwa kwa shirika hilo kwani wamewezesha kuanza mwezi mmoja kabla ya muda uliokuwa umepangwa awali.

Tanesco imefafanua kuwa zoezi hilo limeanza Disemba Mosi, 2023 na kwamba litafanyika kwa siku 10.

Awali zoezi hilo lilipangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Desemba 2023 lakini kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere kumewezesha majaribio kuanza mapema zaidi.

Aidha, Tanesco imesema kwa kipindi chote ambacho zoezi hilo litakuwa likiendelea, kutakuwa na athari za kutokupatikana umeme kwenye baadhi ya maeneo yaliyounganishwa na gridi ya Taifa, kwani njia hiyo ya umeme italazimika kuzimwa kwa siku hizo.

"Kuanza kwa kazi hii ni katika hatua za ukamilishwaji wa Bwawa la Nyerere ambalo litasaidia kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa makali ya mgao wa umeme," sehemu ya taarifa hiyo imeeleza.

Kwa mujibu wa Tanesco hatua zingine zitakazofuata baada ya kukamlishwa kwa zoezi hilo zitakuwa za kuunganisha kituo hicho na njia ya kusafirisha umeme kutoka Luguruni, Dar es Salaam hadi Morogoro,

Pia kuunganisha kituo na njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Ubungo Dar es Salaam, na hatimaye njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze kwenda Tanga.

Kukamilika kwa hatua hizi zote itasababisha kituo kuwa tayari kupokea na kuingiza umeme wa Bwawa la Julius Nyerere kwenye gridi ya Taifa

Imeandikwa na Baraka Loshilaa na Mariam Mbwana