Bwawa la Nyerere lafikia asilimia 91.72 kuanza uzalishaji mwakani

Muktasari:

  • Mradi wa kufua umeme wa katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), umekamilika kwa asilimia 91.72; huku ukitarajiwa kuanza uzalishaji mwakani na hivyo kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Rufiji. Mradi wa kufua umeme wa katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), umekamilika kwa asilimia 91.72; huku ukitarajiwa kuanza uzalishaji mwakani na hivyo kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Mradi huo wenye thamani ya Sh6.6 trilioni, unatarajiwa kuzalisha megawati 2115 za umeme ambao utasaidia kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme nchini ambalo linatokana na upungufu wa maji kwenye mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme.

Leo Septemba 16, 2023, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko ametembelea mradi huo kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Agosti 30, 2023 kuongoza wizara hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kutembelea mradi huo, Dk Biteko amempongeza mkandarasi kwa kasi yake ya kutekeleza mradi huo wa kimkakati pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kwa usimamizi wake wa mradi huo.

"Nimefurahi kwamba mradi umefikia asilimia 91.72 na mkandarasi analipwa kila anapotoa certificate (hati ya malipo) yake. Kwa hiyo katika malipo yote anayodai, ameshalipwa asilimia 85.5 ya fedha zote ambazo ameziandikia certificate," amesema Dk Biteko.

Amesema changamoto ya umeme inayotokana na vyanzo vya maji kupungua, inatarajiwa kumalizwa kutokana na kuwepo kwa mradi huo na kwamba muda siyo mrefu wananchi wataanza kupata umeme wa uhakika na ni imani take kwamba matatizo yalipo sasa ni ya muda mfupi.

"Tuko kwenye hatua za mwisho kuweza kupata umeme wa maana ili kusaidie Watanzania kupata umeme na kuwasaidia kukuza uchumi wao," amesema Biteko wakati wa ziara hiyo katika mradi wa kufua umeme.

Awali akitoa maelezo kwa Dk Biteko, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Emmanuel Mwandambo amesema kwa sasa bwawa limefikia ujazo wa mita 164.81 ambayo ni sawa na lita za ujazo bilioni 14.66, sawa nanasilimia 47.8 ya ujazo wote.

Mhandisi huyo amebainisha kwamba majaribio ya uzalishaji katika mradi huo yatafanyika Februari 2024 wakati uzalishaji kamili ukitarajiwa kuanza Juni 2024.

"Mradi unaendelea vizuri na bwawa limefikia ujazo wa mita 164.81 na hapa tumefungulia maji ili yaendelee kusupport (kusaidia) ikolojia ya viumbe katika hifadhi hii," amesema mtaalamu huyo wakati akielezea mradi.