Bwawa la Nyerere lafikia kina chake, uzalishaji kuanza

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, January Makamba amesema maji katika Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) yamefikia kina cha mita za ujazo 163.61 zinazowezesha uzalishaji kuanza.
Hata hivyo, amesema majaribio ya kuzungusha mitambo yataanza Februari mwakani katika mradi huo utakaoligharimu Taifa Sh6.5 trilioni.
Inatarajiwa ifikapo Juni, 2024 mradi huo utaanza kuzalisha megawati 2,115 za umeme zitakazoingizwa katika Gridi ya Taifa.
Waziri alisema hayo jana, alipozungumza na wanahabari kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, sambamba na ule wa bomba jipya la mafuta kutoka Tanzania hadi Zambia.
Alisema kwa kawaida mita za ujazo zinazohitajika ili kuzalisha umeme ni 163, lakini hadi kufikia juzi walivuka lengo na kufikia kiwango cha mita za ujazo 163.61.
January alisisitiza kuwa kina cha ujazo cha bwawa hilo ni mita 184 kutoka usawa wa bahari na kiwango kinachotakiwa kufikiwa ili kuzalisha umeme ni mita za ujazo 163 kutoka usawa wa bahari.
“Wiki iliyopita tumefanikiwa kujaza maji kiwango kinachotosheleza kuzalisha umeme katika bwawa, maana yake, kuanzia sasa maji yote yanayoingia ni ziada,” alisema January.
“Endapo tungefunga mitambo tungeanza kuizungusha hata leo, lakini kazi inaendelea. Kwa mujibu wa ratiba yetu, Februari mwaka 2024 tutaanza majaribio ya kuzungusha mitambo kwa maji na Juni mwakani tutazalisha umeme.”
Alisema ujenzi unaendelea kwa kasi kubwa hivi sasa, mradi ukiwa umefikia asilimia 89 wakitarajia mwezi ujao watafikia asilimia 90.
Pia, alisema hivi karibuni alikwenda China kuangalia mitambo ya kuzalisha umeme itakayofungwa JNHPP.
“Kifaa cha mwisho cha mitambo kitaondoka China Novemba mwaka huu, maana yake hatua hii itatuwezesha kuwa ndani ya muda. Hii ni habari njema kwa wale waliokuwa na hofu kuwa maji hayatajaa kwa msimu mmoja,” alisema.
Mawaziri sita kukutana leo
Katika hatua nyingine, January alisema mawaziri sita, yeye akiwamo na wengine kutoka Zambia watakutana leo kujadili usalama wa bomba la mafuta na ujenzi wa lingine la gesi.
Mawaziri hao kwa mujibu wa January ni wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa.
Kwa upande wa Zambia watakuwapo Waziri wa Nishati, Peter Kapala, Waziri wa Mambo ya Ndani, Jacob Mwiimbu na Waziri wa Ulinzi, Ambrose Lufuma.
Alisema kikao hicho kitakuwa chini ya uongozi wake na kitatanguliwa na vikao vingine vya wataalamu, wakiwamo makatibu wakuu.
January alisema kikao hicho ni muhimu cha kujadili usalama wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Kigamboni nchini hadi Ndola, Zambia.
Alisema bomba linaloendeshwa na Mamlaka ya Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) lilikuwa likisafirisha mafuta ghafi kwenda Zambia, lakini sasa mfumo umebadilika linasafirisha dizeli.
“Mchakato umekamilika Januari mwaka huu, hivi sasa bomba hilo linasafirisha mafuta ya dizeli badala ya ghafi...kutokana na uamuzi huu mahitaji ya usalama yameongezeka, kwa sababu ni rahisi watu kushawishi kutoboa bomba na kuiba,” alisema.
Alisema katika kikao hicho watapokea taarifa ya utekelezaji wa makubaliano kuhusu ulinzi wa bomba hilo, sambamba na mapendekezo ya ujenzi wa bomba jipya katika eneo hilo hilo.
Alisema biashara ya nishati hiyo imekua na mahitaji ya mafuta yamekuwa makubwa, hivyo bomba la sasa haliwezi kukidhi mahitaji hayo.
“Kumeonekana kuna haja ya kujengwa bomba pana zaidi litakalosafirisha bidhaa nyingine zaidi ya mafuta ya dizeli. Serikali ya Tanzania na Zambia zimekuwa zikiongea kuhusu ujenzi wa bomba hili,” alisema January.
Mbali na hilo, alisema kikao hicho kitajadili mapendekezo ya timu ya wataalamu kuhusu taratibu za kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bomba la gesi na mafuta yatakayotoka Tanzania kwenda Zambia.
Alisema kwa sasa bomba hilo linasafirisha takribani lita milioni 90 kwa mwezi.
January alisema ufanisi wa bomba utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa mafuta sambamba na kuisaidia mikoa ya kusini mwa Tanzania kupata nishati hiyo kwa bei nafuu.