Maji yaliyoibuka chini ya ardhi yazua taharuki Moshi
Muktasari:
- Kwa mara ya kwanza maji hayo yaliibuka mwaka 2020 na kuathiri shughuli za ujenzi wa mradi huo pamoja na makazi ya wananchi yaliyopo pembezoni mwa mradi.
Moshi. Zikiwa zimepita siku zaidi ya 35, tangu kuibuka kwa maji chini ya ardhi katika eneo la mradi wa stendi ya mabasi ya Kimataifa ya Ngangamfumuni, Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe amesema hayajaathiri mradi huo baada ya kuchimbwa visima vitatu kwa ajili ya kuyadhibiti.
Kwa mara ya kwanza maji hayo yaliibuka mwaka 2020 na kuathiri shughuli za ujenzi wa mradi huo pamoja na makazi ya wananchi yaliyopo pembezoni mwa mradi.
Eneo karibu lote lilizingirwa na maji na Serikali ikaagiza wataalam wa miamba kupiga kambi katika eneo hilo ili kunusuru jengo hilo lisimezwe na maji.
Mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2019, ulitarajiwa kukamilika mwaka 2021, lakini utekelezaji wake ulisimama toka mwaka 2020 maji hayo yalipoanza kutoka chini ya ardhi na mpaka sasa hakuna ambacho kinaendelea katika mradi huo.
Hata hivyo, mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh17 bilioni hadi kukamilika kwake na mpaka sasa serikali imeshatoa zaidi ya Sh7 bilioni katika utekelezaji wake ambao umefikia asilimia 43.
Mwananchi imefika eneo hilo na kushuhudia maji yakiendelea kutoka ndani ya eneo la mradi huo ambao umezungushiwa uzio wa mabati na hakuna anayeruhusiwa kuingia huku baadhi ya makazi ya wananchi na barabara zikiwa na maji hayo yanayoendelea kutoka chini ya ardhi na kupasua lami.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe amesema maji hayo hayajaathiri mradi huo na kwa sasa umesimama kutokana na mkandarasi anayeutekeleza kuondoka eneo la mradi.
"Mwaka 2020 maji yalipoibuka, tulichimba visima vitatu vyenye urefu wa mita 60, 50 na kingine mita 30, hivyo tuliyatengenezea maeneo ya kutokea, hivyo jengo letu halijaathrika kwa lolote," amesema Nasombe.
Amesema kwa sasa eneo hilo halina changamoto ya maji kwa kuwa Serikali iliyawekea miundo mbinu mizuri baada ya kufanyika utafiti mbalimbali kutoka kwa wataalam wa miamba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na watalamu wengine waliofika eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha maji hayo hayaathiri mradi huo wa kimkakati.
"Stendi yetu haina changamoto kwa sababu tayari tulishatengeneza miundo mbinu ya haya maji, yanapokuwa mengi yanakuwa na sehemu ya kutokea, pale tulichimba visima vitatu na kisima kinachotoa maji ni kimoja tu kwa sasa, tumeweka pampu, kwa mfano kuna moja tumezamisha pampu mita 60, mita 50 na kingine mita 30 inategemea mkondo kwenye hilo eneo upo eneo gani,” amesema Nasombe.
Kilichokwamisha mradi
Aidha, Nasombe anasema kilichokwamisha mradi huo kuendelea kwa sasa ni mvutano uliopo baina ya manispaa na mkandarasi anayetekeleza mradi huo.
Hata hivyo mkurugenzi huyo anasema wanaendelea na mazungumzo ili kuona ni namna gani anarudi eneo la mradi kuendelea na ujenzi.
"Bado tunaendelea kuzungumzo na mkandarasi, mara ya kwanza alikubali kurejea kwa masharti ambayo manispaa tuliyakubali na tukaanza kumlipa fedha ambazo alitaka kutoka kwetu, lakini kwa makubaliano kwamba akishalipwa zile fedha atarudi eneo la mradi."
"Lakini sasa hivi kaleta tena madai mengine ya Sh300 milioni, hivyo sisi tumeendelea kuwa wapole kwa sababu kazi kubwa ameshaifanya na yeye ndiye anayeujua ule mradi, tunatamani aendelee nao, hivyo tunajaribu kuzungumza naye ili aweze kurudi eneo la mradi na mpaka sasa mradi umegharimu Sh7 bilioni,” amesema mkurugenzi huyo.
Bonde la Pangani
Akizungumzia kuibuka kwa maji hayo, Mkurugenzi wa Bonde la Pangani, Segule Segule, ambaye awali alishiriki kufanya utafiti wa maji hayo amesema, mwanzoni yalipoibuka walifanya tathmini ya kina na wataalamu wengine kutoka Dar es Salaam na walibaini kilichotokea katika eneo hilo ni aina ya miamba iliyopo eneo hilo.
Alisema baadhi ni dhaifu na ilipotikiswa na ujenzi wa jengo hilo, ikasababisha maji kuanza kutoka kwa wingi kutokea ardhini.
“Maji yalipotokea tulifanya tathmini ya kina sisi kama Bonde la Pangani na wataalam wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam na watalamu wengine, tulibaini ni matukio ya kiasili kama ilivyo chemchem, na maji pia hujitokeza kutokana na mpangilio na uimara wa miamba iliyopo eneo husika sambamba na udongo," amesema Segule.
Hata hivyo, anasema bado wanaendelea kulichunguza jambo hilo huku akitoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu kwa sababu kwa sasa maji hayo hayana madhara makubwa.
“Suala hili viongozi wetu wa Wilaya na Mkoa wanalshughulika nalo pia, lakini bado tunaendelea na ufuatiliaji, tutawashauri kitaalamu na wao watafanya maamuzi na kuona ni hatua gani zichukuliwe, lakini kwa sasa bado hatujaona madhara makubwa zaidi ya usumbufu wa maji kujaa kwa kiasi kwenye makazi ya wananchi,” amesema.
Wananchi wafunguka
Loti Saitoti mkazi wa Mfumuni, amesema hali si nzuri hasa ikizingatiwa eneo hilo kunajengwa mradi mkubwa wa stendi ya mabasi.
“Tunaomba Serikali ione njia gani ya kuyadhibiti haya maji, iongeze nguvu katika kutafuta suluhisho la haya maji, wasiwasi wetu ni pale tunposhuhudia maji haya yakitoka ardhini kwa wingi, tunajiuliza hayawezi kuleta madhara makubwa, kwa sababu hatujaelezwa chochote na hatuelewi suluhisho ni nini,” amesema mkazi huyo.
Deogratius Kimario amesema maji hayo ambayo ni takribani mwezi na nusu umepita tangu yaanze, hawajui suluhisho lake hali inayozidi kuibua kuibua hofu miongoni mwao.
“Hii ni mara ya pili tatizo hili linatokea, lilitokea tena miaka mitatu iliyopita, viongozi wanakuja lakini hawatuelezi wananchi tatizo ni nini, hatujui ufumbuzi wake itakuwa ni nini, tunaomba serikali itusaidie kutuma watafiti wake wachunguze wajue tatizo ni nni na kuona mwamba unaotoa maji kama kutakuwa na suluhisho,” amesema Kimario na kuongeza;
“Tuko gizani, hatujui nini kinachoendelea na eneo hili kama mnavyoona kuna mradi mkubwa wa stendi ya kimataifa, ndani walichimba kisima, kimejaa maji na ndiyo yanatoka nje, lakini pia maji haya yanatoka kwenye nyumba za watu na wengi yamewaathiri.”