Maji yanayotoka Bwawa la Nyerere yaendelea kuwatesa Rufiji, 55 wajihifadhi shule

Muktasari:

  • Mafuriko yaliyoikumba Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kutokana na maji kufunguliwa kutoka Bwawa la Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) yameendelea kusababisha adha kwa wananchi.

Rufiji. Mamia ya wananchi hawana mahali pa kuishi, huku wengine 55 kutoka kaya 15 wakihifadhiwa kwenye shule za msingi wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, baada ya nyumba zao kufunikwa na maji yanayotoka katika Bwawa la Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).

 Mbali na kukosa makazi, wananchi hao wako hatarini kukumbwa na njaa, baada ya mazao yao kuzama kwenye maji shambani.

Mwananchi Digital limeweka kambi Rufiji, Mkoa wa Pwani kuangazia kinachoendelea juu ya athari zinazotokana na mafuriko hayo.

Leo Alhamisi Aprili 4, 2024 katika Kijiji cha Mohoro wilayani humo, Diwani wa Mohoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rufiji, Abdul Chobo amesema tathimini za kila siku zinaonyesha maafa yanaendelea kuongezeka.

"Watu wote wamehamia kwa ndugu, ila kwa leo hii tumepata watu waliokosa makazi wamekimbilia kwenye shule kama kaya 15 zina watu takriban 55," amesema.

Hata hivyo, amesema wamewataka watu hao watafute sehemu nyingine kwa kuwa Jumatatu ya Aprili 8, 2024 shule zinafunguliwa.

"Hao watu wanajihudumia wenyewe kwa asilimia 100 kwa chakula na malazi, kwa sasa tunafanya tathimini ili kujua mahitaji, kwani kwa hali ya sasa huwezi ukaleta viroba 50 au 100 halafu ugawe, utamgawia nani umuache nani, ni lazima tuangalie wako wangapi," amesema.

Amezitaja shule zinazowahifadhi kuwa ni Mohoro na Nyampaku na kuongeza kuwa hakuna kifo kilichotokea tangu mafuriko yalipoanza.

Akizungumzia ujio wa Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, Chobo amesema kiongozi huyo amebadili matumizi ya Sh40 milioni alizotenga kwa ajili ya kufuturisha, sasa zitumike kununua mbegu za mazao kwa wakulima.

"Tunamshukuru mbunge wetu Waziri Mohamed Mchengerwa aliyekuja kutuangalia na kuwapa moyo wananchi kwamba watulie.

"Zile fedha Sh40 milioni amezileta, ili kununua mbegu za mazao kwa kuwa mashamba yamezama kwenye maji. Kwa hiyo maji yatakapopungua, watu hawa watajitetea kwa kupanda mbegu hizo, ili kupata chakula.

"Mheshimiwa Waziri amemwagiza mkuu wa wilaya kufanya tathimini ya maafa haya, ili kupeleka kitengo cha maafa tupate msaada. Kwa sasa mazao kama ndizi, mahindi, mpunga vyote vimeangamia kwenye maji," amesema.

Ameendelea kusema kabla ya mafuriko hayo, mkuu wa wilaya hiyo alitoa tahadhari kwa kuweka mabango, lakini wananchi waliohama walikuwa wachache.

"Wapo wachache waliotoka, lakini wengi hawakutoka kwa sababu watu hasa wa Rufiji wamezoea maji, hivyo hawakuamini," amesema.

Kata ya Mohoro ina vijiji sita na vijiji vinne vimezama kwenye maji. 

Wakizungumza na Mwananchi Digital katika eneo la kivuko, baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuharakisha msaada.

Mariam Mtulia, mkazi wa Mohoro, amesema mbali ya nyumba yake kuzama, hata biashara yake ya mamalishe imekwama.

"Maji haya yametujia ghafla, ndio tunapata adha hii hivyo tunaomba msaada.

“Kwa biashara zangu hizi za chakula, napata tabu kwa sababu ya maji. Nyumba yangu imezama, hivyo nimejihifadhi kwa ndugu," amesema.

Kwa upande wake, Sultan Powa amesema msaada wa haraka unahitajika.

"Tunaomba Serikali ituambie hatima yetu itakuwaje maana hadi sasa hatujui hali itakuwaje.

"Kabla ya kuja haya maji kulikuwa na daraja tulilotumia kuvuka kwenda kwenye makazi yetu, lakini kutokana na hali hii tunashindwa kutumiza mahitaji yetu, tunalazimika kutumia mitumbwi ya kulipia kwenda kwenye vijiji vyetu,” amesema na kuongeza;

"Haya maji ni ya mvua, lakini haya yametokana na kufunguliwa kwa Bwawa la Julius Nyerere na tumeambiwa yatakwisha Mei 25, 2024, hivyo tunaomba msaada wa haraka."

Naye Ally Kaniki kutoka kijiji cha Shera, amesema wamepoteza mazao yote yaliyokuwa shambani.

"Nimekwenda kuangalia shamba langu maji yanafika kifuani, mazao yote yamezama.

"Hali hii pia inatuweka kwenye hatari ya magonjwa kwa sababu nyumba zote zimefunikwa na maji, hivyo tutapa magonjwa. Hata miguu nayo inapata fangasi ndio maana tunapaka oili," amesema.

Hata hivyo, Hanafi Simba ambaye ni nahodha wa mtumbwi amesema huu ni wakati wa neema, kwani abiria wameongezeka.

"Hizi ni changamoto za kimaisha, ni mambo ya Mwenyezi Mungu. Kwa siku navusha watu 80, kwa sababu chombo changu kinachukua abiria 20 na kila mtu analipa Sh200. Ni kusaidia tu, maana wengi wameathirika," amesema.