Prime
Makada Chadema, mhadhiri UDOM kortini kwa ugaidi
Muktasari:
- Washtakiwa hao wameshtakiwa katika mahakama tofauti, wote wakikabiliwa na shtaka moja la ugaidi, wakidaiwa kushiriki katika vitendo vya kigaidi kwa tarehe na maeneo tofauti.
Dar/Mbeya/Mwanza. Makada zaidi ya 20 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamepandishwa kizimbani katika mikoa na mahakama tofauti na kusomewa mashtaka ya ugaidi na uhujumu uchumi.
Miongoni mwa washtakiwa hao, wamo wanafunzi wanne wa vyuo vikuu tofauti mkoani Mbeya, wengine jijini Mwanza huku mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma akifunguliwa mashtaka kama hayo mkoani Dodoma.
Wanafunzi hao walioshtakiwa kwa kosa hilo lisilo na dhamana, ni Noah Mwalwange (23), mkazi wa Isange na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Gwamaka Mboka (28), Rojazi Mpwani (21) na Augustino Wasinyo (25), wote wa Chuo Kikuu cha Katoliki (CUoM).
Wanafunzi hao kwa pamoja walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Paul Rupia wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya, jana Alhamisi, Julai 23, 2026 na kusomewa shtaka la kushiriki katika vitendo vya kigaidi.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na vifungu namba 4(1), (2) na (3)(c); 31(d) vya Sheria ya Kuzuia Ugaidi (Sura ya 19, Marejeo ya Mwaka 2023), vikisomwa pamoja na Aya ya 24 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 61(2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kupanga na Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Marejeo ya Mwaka 2023).
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wanafunzi hao wanadaiwa kuwa walitenda kosa hilo Julai 4, 2026, katika eneo la Mafiati, jijini Mbeya.
Wanadaiwa kuwa siku hiyo kwa pamoja walishiriki katika vitendo vya kigaidi kwa kuwashawishi watu katika eneo hilo la Mafiati kutenda vitendo vya kigaidi vinavyohusisha uharibifu mkubwa wa mali kwa lengo la kuwatisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali na wanafunzi hao, Jasiri Mwasumbi (29), mkazi wa Kalombe, naye alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa shtaka hilohilo la kushiriki katika vitendo vya kigaidi mbele ya Hakimu Tedy Mlimba.
Jasiri ambaye ni dereva anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 5, 2026, katika eneo la Kalombe. Anadaiwa kuwa siku hiyo, katika eneo hilo, alishiriki katika vitendo vya kigaidi kwa kuwahamasisha watu kutenda vitendo vya kigaidi vinavyohusisha kuwashambulia askari polisi mkoani Mbeya ili kusababisha vifo au majeraha, kwa lengo la kuwatisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakili Philipo Mwakilima anayewatetea washtakiwa hao amelieleza Mwananchi kuwa wanafunzi na dereva huyo walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka jioni, baada ya yeye kuwa ameondoka mahakamani na kwamba kesi zote zitatajwa Agosti 6, 2026.
Makada wa Mwanza
Katika hatua nyingine, washtakiwa 23 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza wakishtakiwa katika kesi mbili tofauti za kujihusisha na mikutano au mazungumzo yanayoweza kusababisha ugaidi.
Baadhi ya washtakiwa hao ni viongozi wa Chadema na kesi zao zimesomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Naibu Msajili Erick Marley.
Katika kesi ya kwanza namba 16379/2026, washtakiwa 13 kutoka Wilaya ya Ilemela wanashtakiwa kwa kufanya kosa hilo kati ya Juni 25 hadi Julai 7, 2026.
Washtakiwa hao ni Alphaxadi Nyamwaga, Fantson Mpango, Abely Mwesa, Hassan Said, Emmanuel Wambura, Adam Idd, Damas Sadock, Petro Mabula, Abdul Kagwidi, Devid Mashaka, Philipo Masatu, Edward Mikindo na Emmanuel Doto.
Kesi ya pili namba 16375/2026 imewahusisha washtakiwa 10 kutoka Wilaya ya Nyamagana ambao pia wanashitakiwa kwa kufanya mikutano hiyo kati ya Julai 4 hadi Julai 7, mwaka huu, katika eneo la Igoma.
Washtakiwa hao ni Deus Masalago, Mohamed Tosha, Fabian Nguvumali, Samweli Mtani, Samweli Kobell, Julius Makonga, Fanuel Lutana, Philipp Kulwa, Philipp Shipuluko na Hamis Mnyimvua.
Washtakiwa hao wanatuhumiwa kufanya vikao hivyo vyenye lengo la kufanya ugaidi, wakiwa na lengo la kupanga kuchoma moto majengo ya Serikali na ya binafsi.
Watuhumiwa wote wamerudishwa rumande kwa kuwa Mahakama hizo hazina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, ambayo imepangwa kutajwa Agosti 6, 2026.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili anayewatetera, Erick Mutta amesema watuhumiwa hao walikuwa wanashikiliwa mahabusu kwa takribani mwezi mmoja hadi jana walipofikishwa mahakamani hapo.
Amesema washtakiwa hawakudhaminiwa kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya ugaidi, hivyo wamerudishwa rumande.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadi, kati ya watuhumiwa hao 23, wanane ni viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho kuanzia kata hadi matawi katika wilaya za Nyamagana na Ilemela.
Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Gaston Garubindi amesema hadi sasa makada na viongozi 27 wa mikoa ya Mwanza na Mbeya wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi.
“Ingawa wapo wengine wanaoendelea kushikiliwa kwenye vituo vya polisi vya mikoa ya Dar es Salaam, Iringa na Shinyanga, hawa 31 wamefikishwa mahakamani na kusomewa makosa ya ugaidi.
“Dar es Salaam wanashikiliwa wanne, Iringa watatu, Kishapu (Shinyanga) wapo saba ndani,” ameeleza Garubindi.
Pamoja na hayo, Garubindi amesema timu ya wataalamu wa sheria wa chama hicho bado inaendelea na mchakato wa kuhakikisha viongozi na makada hao wanapata dhamana.
Mhadhiri UDOM
Katika hatua nyingine, baada ya kushikiliwa na polisi mkoani Dodoma kwa siku 15, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedek Kaijage pia amefikishwa mahakamani jijini Dodoma akishtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi na ugaidi.
Mhadhiri huyo alifikishwa mahakamani Julai 23, 2026, na kusomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule, na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 5, 2026, itakapotajwa.
Kaijage alikamatwa Julai 8, 2026, akituhumiwa kuhamasisha maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Julai 7, 2026, siku ya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (DITF), maarufu Sabasaba, ambayo kwa sehemu kubwa huadhimishwa jijini Dar es Salaam.
Julai 23, 2026, mhadhiri huyo, aliyekuwa akishikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Chang'ombe jijini Dodoma, alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo.
Kosa aliloshtakiwa nalo linaangukia katika Kifungu cha 4(1), (2)(a) na (3)(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi, Sura ya 19, Toleo la mwaka 2023, kikisomwa pamoja na Aya ya 24 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 61(2) vya Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa Julai 3, 2026, katika eneo la UDOM, anadaiwa kutenda kosa la kigaidi, ambalo ni kinyume cha sheria za Tanzania.
Kulingana na maelezo ya Jamhuri, anadaiwa kutishia kuchoma moto majengo ya umma na makazi ya polisi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuwatisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mshtakiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu lolote, ataendelea kushikiliwa mahabusu kwa kuwa kosa hilo halina dhamana na mahakama alikosomewa mashtaka haina mamlaka ya kulisikiliza.