Prime
Makada wa CCM katika vita ya kutaka uenyekiti

Mchungaji Jacob Mwakasole (kushoto) akirejesha fomu ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti Mkoa wa Mbeya. Picha na Hawa Mathias.
Mikoani. Mbio za uchaguzi wa wenyeviti wa CCM katika mikoa mitatu ya Mbeya, Arusha na Mwanza, zimezidi kushika kasi huku vigogo wakitajwa kuchuana katika kinyang’anyiro hicho.
Nafasi za wenyeviti wa CCM katika mikoa hiyo iko wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo cha mmoja wao na wengine wawili wakiteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen alifariki Oktoba 27, mwaka huu wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Mbeya, Stephen Mwakajumilo akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu na mwenzake wa Mwanza, Sixbert Jichabu akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.
Tayari mchakato wa kujaza nafasi hizo umeanza huku vigogo wakitajwa kuchuana kwenye kinyang’anyiro hicho zikiwa ni mbio kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mkoani Mbeya
Katika Mkoa wa Mbeya, jumla ya makada 21 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania uongozi wa chama katika mkoa huo, ambapo kati ya hao, watatu ni wanawake.
Miongoni mwa watia nia hao, vigogo kadhaa wanatajwa kuongeza joto kwenye uchaguzi huo.
Baadhi ya wanaowania nafasi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya kati ya mwaka 2017 na 2022, Mchungaji Jacob Mwakasole anayetafuta kurudi.
Katibu Mwenezi mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile alimtaja kada mwingine aliyechukua fomu kuwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya, Humphrey Msomba, huku akieleza kuwa wote waliojitokeza wana sifa za kuwa viongozi ndani ya chama.
Uhavile alisema bado makada wenye nia ya kugombea nafasi hiyo wanakaribishwa na kwamba shughuli hiyo itafungwa rasmi Novemba 16, mwaka huu.
“Kikubwa kama chama tumepiga marufuku na kutahadharisha wagombea kutojihusisha na kampeni kabla ya wakati kufika,” alisema.
Mkoani Mwanza
Huko mkoani Mwanza, hadi kufikia jana, ni aliyekuwa katibu mwenezi CCM mkoa wa Mwanza, Simon Mayunga maarufu kama Mangelepa ndiye alithibitishia kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea uenyekiti wa chama hicho mkoani Mwanza.
Uchaguzi huo unafanyika kujaza nafasi iliyobaki wazi baada ya aliyekuwa Mwenyekiti, Sixbert Jichabu kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Katibu wa CCM Mkoa, Omari Mtua alisema hayupo katika nafasi nzuri ya kutoa taarifa za wanachama waliochukua fomu jana kutokana na kuwa kwenye ziara ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Paul Makonda mkoani humo, lakini Mayunga alithibitisha kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kurejesha ama mchuano wa moja kwa moja kati ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Dk Anthony Diallo na mkuu wa mkoa wa zamani, Said Mecky Sadiki ambao wametokea kuwa washindani wakuu tangu uchaguzi wa mwaka 2017 ulioshuhudia Dk Diallo akiibuka mshindi.
Mkoani Arusha
Kwa upande wa Arusha, chama mkoani humo kimesema kinasubiri muda wa kikatiba wa siku 60 kwa ajili ya kutangazwa kwa uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha.
Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Saipulani Ramsey, alisema kwa sasa wanasubiri utaratibu.
“Utaratibu ni kwamba kiongozi akifariki, akiondoka kwa kuteuliwa au kuvuliwa uanachama, mnakaa siku 60, kwa hiyo maeneo mengine walishakaa siku 60 ndiyo maana wanaruhusiwa kufanya uchaguzi. Arusha bado tunalia na mwenyekiti wetu.
Imeandikwa na Hawa Mathias, Janeth Mushi na Peter Saramba.