Makalla aanza ziara Dar, kinachomsubiri hiki hapa

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla
Muktasari:
- Baada ya jana Jumapili Julai 6, 2024 kufanya kikao cha ndani na viongozi na wanachama wa CCM mkoani Dar es Salaam, leo Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla ataanza ziara rasmi ya kutembelea wilaya tano za mkoa huo.
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla leo Jumapili Julai 7, 2024 ameanza ziara ya kukagua uhai wa chama hicho katika wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam, akianzia Ilala ambako huenda akakumbana na kilio cha miundombinu ya barabara.
Katika ziara hiyo ya siku sita, Makalla atatembelea pia wilaya za Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke mbali na kuangalia mwenendo wa chama hicho, atapata fursa pia ya kufanya mikutano ya hadhara ili kuwasikiliza wananchi na kuchukua kero zao.
Kabla ya kuanza kwa ziara hiyo, jana Jumamosi, Julai 6, 2024, Makalla alikutana na wanachama na viongozi wa CCM katika kikao cha ndani na kueleza mipango mbalimbali ikiwemo kuhakikisha chama hicho kinaibuka kidedea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, utakaofanyika baadaye mwaka huu. Pia, Makalla ni mlezi wa chama hicho, Mkoa wa Dar es Salaam.
Kero kubwa katika wilaya ya Ilala ambayo Makalla na ujumbe wake watakutana nayo ni kilio cha miundombinu hasa barabara katika maeneo ya Majohe (haina barabara ya lami), Vingunguti, Kivule, Msongola na Zingiziwa
Suala la miundombinu ya barabara kimekuwa kilio kwa wakazi wa jiji la Dar ea Salaam, wakati katika masuala ya chama atakumbana na changamoto ya upatikanaji wa kadi za kieletroniki zinazotoka kwa awamu huku mahitaji yakiwa makubwa.
Sasa hivi kilio cha huduma za afya au shule kimepungua kutokana na Serikali kujenga vituo vya afya na shule karibu na wananchi ili kuwarahisishia huduma hizo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Julai 7,2024 Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto amesema kwa sasa halmashauri hiyo, imetengewa asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya miundombinu , hawatakiwi kuzidi hapo.
"Watu wana kiu kubwa na mradi wa DMDP (Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Dar es Salaam) utakaotibu kiu ya wananchi wa jiji hilo.
"Kilio kikubwa na barabara hasa za kiwango cha lami, lakini sheria na miongozo inatutaka ni asilimia 10 ya mapato yetu kila mwaka, maana yake ukisema fedha zote ziende kwenye barabara hautaweza kutoa mikopo ya asilimia 10,"amesema Kumbilamoto ambaye ni diwani Vingunguti.
Kumbilamoto amesema baadhi ya maeneo atakayotembelea Makalla ni pamoja na kukagua miundombinu ya huduma za jamii zikiwemo shule na vituo vya afya, ambapo atajionea utekelezaji wa Ilani ya CCM ulivyokwenda.
Akiwa Wilaya ya Ilala kiongozi huyo atatembelea na kukagua tenki la maji la Bangulo kata ya Ukonga, Shule ya Msingi Tungini (Chanika), Shule ya Msingi Minazi Mirefu na kituo cha afya Kinyerezi.