Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makalla ataka wazalishaji kuongeza tija kufikia Dira 2050

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake leo Jumatano Juni 24,2026 kuhusu maandalizi ya maonyesho ya Nanenane ambayo kwa Kanda ya Kaskazini yatafanyika viwanja vya Themi,Njiro jijini Arusha.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amesema Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini mwaka huu yatajikita katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki ili kuongeza tija katika uzalishaji, kuimarisha ushindani wa bidhaa na kuchochea ukuaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani ili kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amewataka wakulima, wafugaji na wadau wa uzalishaji kuongeza tija katika uzalishaji ili kuendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukuza uchumi wa vidogo na vya kati vinavyotumia malighafi za kilimo na mifugo ya hapa nchini.

Makalla amesema hayo leo Jumatano Juni 24, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya maonyesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) ambayo kwa Kanda ya Kaskazini yatafanyika Viwanja vya Themi, Njiro jijini Arusha kuanzia Agosti Mosi hadi nane,mwaka huu.

Amesema kuwa maonyesho ya mwaka huu yatakuwa tofauti na miaka mingine kutokana na kuzingatia zaidi matumizi ya teknolojia na ubunifu katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki.

Amesema wananchi wataona na kujifunza  teknolojia za kisasa za kilimo,mbegu bora za mazao, mbinu za kuongeza usalishaji, ufugaji bora na matumizi ya nishati safi lengo likiwa ni kuongeza tija katika uzalishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Mkuu huyo amesema kaulimbiu ya mwaka huu inasema "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050" inalenga kuwahamasisha wazalishaji kuelekeza nguvu katika uzalishaji wenye tija unaokidhi mahitaji ya soko na kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati.

“Tunataka wakulima wetu, wafugaji wetu na wavuvi wetu waongeze tija. Dira ya 2050 inaelekeza taifa kuwa na uchumi unaotegemea uzalishaji wenye thamani kubwa. Hii haiwezekani bila kuwa na malighafi za kutosha kutoka katika sekta za kilimo na mifugo ambazo ndizo zitakazosaidia ukuaji wa viwanda vidogo na kuongeza ajira kwa wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Arusha ambaye pia ni mmoja wa waratibu wa maonesho hayo Kanda hiyo,  Daniel Loiruk, amesema mwaka huu  kutakuwa na teknolojia mpya na za kisasa zinazolenga kuongeza tija na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Loiruk ametaja  miongoni mwa teknolojia hizo ni matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone) katika kilimo, mifumo ya ufuatiliaji wa afya ya udongo, teknolojia za kutambua na kufuatilia mifugo kwa njia za kidijitali pamoja na mashine za kisasa za kutengeneza malisho ya mifugo.

“Mwaka huu tutakuwa na teknolojia nyingi ambazo hazikuwahi kuonekana kwa kiwango hiki katika maonyesho yaliyopita.

“Zipo teknolojia za kufuatilia afya ya udongo, matumizi ya drone katika kudhibiti visumbufu vya mazao, pamoja na mifumo ya kisasa ya utambuzi wa mifugo inayowezesha wafugaji kufuatilia taarifa muhimu za mifugo yao,” amesema.

Amesema pia kutakuwepo na teknolojia za ufugaji wa samaki ikiwemo mashine za kutotolesha vifaranga vya samaki na teknolojia za chanjo kwa ajili ya kuboresha uzalishaji katika sekta hiyo.

Amesema sekta ya ufugaji nyuki nayo itakuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya maonyesho hayo kutokana na kuoneshwa kwa teknolojia mpya za uzalishaji wa asali, nta, gundi na uvunaji wa sumu ya nyuki inayotumika katika matibabu na shughuli nyingine za kiuchumi.

“Sekta ya nyuki nayo itapata nafasi kubwa ambapo kutakuwepo na teknolojia za kisasa za uzalishaji wa asali,nta,gundi na sumu ya nyuki inayotumika katika tiba na bidhaa mbalimbali za viwandani. Mifumo ya kidijitali inayomwezesha mfugaji kufuatilia hali ya mizinga kwa njia ya simu bila kuwa eneo la tukio,“ amesema.

Amesema maonyesho hayo pia yataweka mkazo kwenye matumizi ya nishati safi kupitia maonesho ya pampu za maji zinazotumia gesi, mifumo ya kupikia inayotumia nishati mbadala na teknolojia mbalimbali zinazosaidia kupunguza matumizi ya nishati chafu.