Makalla awaonya wanaonunua viwanja bei chee Dar

Muktasari:

Makalla ameyasema hayo alipokuwa akieleza hatua zilizochukuliwa katika mgogoro wa ardhi katika eneo la Mabwepande, ikiwa pamoja na kuunda kamati iliyo nyaraka za uhalali wa umiliki ardhi kwa wananchi wapatao 3,988.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewatahadharisha wakazi wa mkoa huo kutokimbilia kwenye viwanja vya bei nafuu, akisema aina na viwanja hivyo mara nyingi vinauzwa kiutapeli.

Makalla ameyasema hayo jana Agosti 10 alipofanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mabwepande, akiwaeleza hatua zilizochukuliwa kwa wavamizi wa maeneo ya watu na taasisi za umma katika kata hiyo.

Amesema kufuatia migogoro ya ardhi kwenye hilo, aliunda iliyofanyankazi kwa miezi miwili na imempelekea mapendekezo 19 ya kutafuta suluhu ya tatizo hilo, baada ya kukagua nyaraka za uhalali wa umiliki ardhi kwa wananchi wapatao 3,988.

"Naomba niwaambie wananchi wa ndani na nje ya Dar es Salaam hakuna ardhi katika jiji hili inayozwa kwa Sh300,000 na ukinunua ujue umeibiwa tu," alisema Makalla.

Kuhusu maeneo yaliyovamiwa, Makalla amesema wameanza kushughulika na taasisi za serikali ikiwemo ya Shirika la Maendeleo Dar es Salaam (DDC), ambalo lina jumla ya ekari 5,000 na lile la linalomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambao nao wana ekari 168.

"Maeneo yote haya tumekubliana wavamizi kurasimishwa kwa kupimiwa na kuuziwa na vingine vitauzwa kwa watu mbalimbali kwa ajili ya makazi na biashara," amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya DDC, Abbas Mtemvu, alishukuru mgogoro huo kuisha na kueleza kuwa kwa mwaka walikuwa wakitumia Sh20 milioni katika kufuatilia mgogoro huo huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa wananchi wa eneo hilo.

Akizungumzia hatua hiyo, Meya wa Kinondoni, Sengoro Mnyonge amesema baada ya watu kumilikishwa maeneo wangependa kuona Mabwepande kunajengeka kwa mpangilio na kuwa mji wa mfano.

Awali Kamshina wa ardhi mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kahyera, amesea licha ya mgogoro katika eneo hilo kumalizwa kuna baadhi wameendelea kuwa wakaidi wakirudi kujenga nyumba za muda ambapo alionya hao hawatavumiliwa.

 Baadhi ya wananchi wa Mabwepande, wamepongeza hatua hiyo wakisema itaondoa mzozo wa muda mrefu.

Mariaclara Hizza, alisema walau sasa atalala usingizi na kueleza kwamba kwa kipindi cha miaka minne tangu ahamie eneo hilo amekuwa akiishi kwa wasiwasi haswa wanapoona magari ya serikali yakipita.

Naye Faraja Kikoto, aliahidi kuwa watakuwa walinzi wenyewe kwa wenyewe kuhakikisha hakuna wengine wanaovamia kwa kuw tayari orodha ya wakazi wa eneo hilo serikali inayo.