Makalla: Kuna wanaume wananyanyaswa na wanawake wenye fedha

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salama, Amos Makalla amesema pamoja na kupokea kero za wanawake wanaokutana na unyanyasaji wa kijinsia wapo wanaume wanaohitaji msaada kutokana na changamoto za aina hiyo.

  

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salama,  Amos Makalla amesema pamoja na kupokea kero za wanawake wanaokutana na unyanyasaji wa kijinsia wapo wanaume wanaohitaji msaada kutokana na changamoto za aina hiyo.

Akizungumza leo Alhamisi Novemba 25, 2021 wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, Makala amesema sasa hivi wanaume wamekuwa na malalamiko dhidi ya wanawake wenye fedha.

“Nilikuwa na ziara ya kusikiliza kero za wananchi, asilimia 30 ya kero 927 nilizopokea zinatokana na changamoto za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia."

“Kwenye kero nilizozikuta wapo wanaume wanaonyanyaswa. Kuna wanawake wana fedha wanahitaji tu wanaume wa kuwaoa, hivyo anaweza kumpa kitu mwanaume na kumnyang’anya punde wakiachana,” amesema Makalla.

Mkuu huyo wa mkoa ameongeza, “Nimeyaona hayo wale wanaume marioo waliozoea kitonga  wanakuja ofisini kulalamika kuwa walipewa mali na wanawake lakini wakanyang’anywa.

“Sasa swali linakuja hii sio ukatili? Naona kuna mjadala mpana katika hili suala la unyanyasaji wa kijinsia ndio mana mjadala mzuri wenye lengo la kuboresha sheria za ndoa,”.