Makalla na onyo kwa 'Panya Road'
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla
Muktasari:
Wakati kikundi cha panya road kikiendelea kuzua hofu kwa uhalifu jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ametangaza operesheni kuanzia juzi usiku kuwa “hakuna atakayeonewa huruma.”
Dar es Salaam. Wakati kikundi cha panya road kikiendelea kuzua hofu kwa uhalifu jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ametangaza operesheni kuanzia juzi usiku kuwa “hakuna atakayeonewa huruma.”
Wiki iliyopita Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilitangaza kuwakamata vijana 10 wanaohusishwa na kundi hilo baada ya kujeruhi watu 19 maeneo ya Tabata na Chanika pamoja na kuwapora mali zao.
Kama haitoshi, kundi hilo juzi lilivamia eneo la Mjimpya Kunduchi na kujeruhi watu 19, huku wakipora pesa, simu, pombe na sigara katika maduka.
Hadi jana jioni, kamanda wa kanda hiyo maalumu, Jumanne Muliro alisema wanawashikilia vijana sita wanachama wa panya road waliovamia maeneo ya Kunduchi ili waeleze wenzao wako wapi, kwa nini wanafanya matukio hayo na vitu wanavyopora wanavipeleka wapi.
Operesheni
Kufuatia matukio ya kundi hilo yanayojenga hofu katika jamii, Makalla ametangaza operesheni ya kukabiliana nalo.
Operesheni hiyo inakuja siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kulionya kundi hilo alipohutubia sherehe za Mei Mosi jijini Dodoma akisema linahatarisha maisha ya wananchi na yao wenyewe.
Katika mkutano wake na vyombo vya ulinzi na usalama uliowashirikisha wakuu wa wilaya zote tano, Makalla aliwatoa hofu wakazi wa mkoa huo akieleza kuwa operesheni hiyo haitamuonea mtu zaidi ya kudhibiti uhalifu na kuvunja mtandao wa panya road.
“Panya road hawawezi kukaa hapa na kuwakosesha watu raha kwa bisibisi na mapanga. Sasa iko hivi, kama unatumia panga itatumika silaha kubwa zaidi kukunyang’anya hilo panga maana lengo lao ni kuua.
“Tunaanzisha operesheni kabambe kupambana nao, hatutoruhusu watambe na bisibisi na mapanga mtaani. Kuanzia usiku wa leo na kuendelea hakuna panya road atabakia katika mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Makalla.
Mkuu huyo wa mkoa aliyataja mambo matano ya kuzingatiwa katika operesheni hiyo kwa kamati za ulinzi na usalama za wilaya kukaa na wenyeviti wa mitaa kuangalia namna ya kudhibiti uhalifu kwenye mitaa yao.
Pia ameagiza kuongezwa kwa doria katika mitaa kwa wakuu wa wilaya kuanzisha mpango wa kuwatumia askari mgambo katika kuimarisha ulinzi.
Amelitaka pia Jeshi la Polisi kuhakikisha linawasaka na kuwakamata wanunuzi wa mali zilizoibwa na panya road na kutoa taarifa ya operesheni hiyo.
Wafanya kufuru
Wakati operehseni hiyo ikianzishwa, kundi hilo limevamia Kata ya Kunduchi na kujeruhi watu 19 na kuwapora mali.
Grace Michael, mmoja wa majeruhi wa tukio hilo aliyekatwa kwa panga kisogoni, mkononi na mgongoni alisema alivamiwa ghafla.
“Nilikuwa nimeenda kuweka muziki katika flashi, wakati nampa yule kaka flashi yangu nilisikia kelele ya vijana wakisema wezi wengine ndiyo hawa, nikiangalia nipo mimi na huyu kaka pekee sasa wakati najiuliza nini kinaendelea mwenzangu alikimbia.
“Mimi nikiwa natafuta njia ya kupita nilipigwa panga nyuma ya kichwa, lingine mgongoni na wakati nakimbia nilirusha mkono likaukata,” alisema Grace.
Alisema hali hiyo ilimfanya atafute njia ya kujiokoa ili aombe msaada katika nyumba iliyokuwa ya jirani.
Saa tatu usiku maduka mengi yakiwa hayajafungwa, kundi hilo lilipora fedha katika duka alilokuwapo Grace kabla ya kuhamia dukani jirani walikomkuta Hamad Abdallah, wakamshambulia pia.
Kijana huyo (16), alikatwa panga karibu na utosi alipovamiwa na vijana watatu waliotaka fedha.
“Walichukua hela zote zilizokuwepo dukani na kuondoka nazo,” alisema Abdallah.
Wakati hilo likitokea, mmiliki wa duka analouza Abdallah, Saju Ramadhani alijeruhiwa kwa chupa mguuni aliyasahau maumivu yake alipoona kijana wake akivuja damu nyingi za majeraha.
“Inavyotokea ni kwamba wanakuja wengi na wanapiga kelele za mwizi, sasa walipokuwa wanakuja wakiita mwizi huyo kijana tunamfahamu sasa mmoja akasema tunamjua huyu siyo mwizi akageuziwa kibao na kuanza kupigwa ndipo wote tulishtuka na kukimbia,”
“Sasa tulikuja kushtuka kuwa huyu dogo (Abdallah) tumemuacha dukani ilikuwa ni muda umepita na wote tunaogopa kutoka, yeye baada ya kuwa amejeruhiwa na haoni msaada ukija aliamua kuja ndani wote tulichanganyikiwa kumuona,” alisema.
Katika tukio hilo, Ramadhan alipoteza mauzo ya maduka matatu anayoyamiliki kwa alichokieleza kuwa duka lililovamiwa ndilo hujumuisha mauzo yote.
“Hadi sasa sijui ni kiasi gani kimepotea maana nilikuwa nimeweka humo ndani mauzo ya wiki nzima katika maduka yangu na nilitarajia leo (jana) nipige hesabu nikachukue mzigo,” alisema Ramadhani.
Diwani wa Kunduchi, Michael Urio alisema waliwaialiana na Jeshi la Polisi ambalo lilifanya operesheni ya kuwasaka waliotekeleza tukio hilo.
“Jana nilikuwa nao hadi usiku kuendelea kufuatilia maeneo yaliyoathirika ikiwemo Mtongani na Mji Mpya na watu walioumizwa hadi sasa ni 19,” alisema Urio.
Diwani huyo alisema ana imani waliotekeleza unyama huo si wakazi wa eneo hilo na walikuwa kwenye makundi wakiwa wanafuatana.
Kuhusu vikundi vya ulinzi shirikishi alisema vipo katika kata yake lakini muda wa tukio ilikuwani bado mapema sana.
Ulinzi waimarishwa
Katika mitaa ya Kisiwani na Twiga Tabata ambako yameripotiwa matukio ya panya road kuvamia viongozi wake walisema wameimarisha ulinzi wa kutosha kwa kushirikiana na kuweka vizuizi barabarani.
Mtendaji wa Mtaa wa Kisiwani, Shekha Mandwa alisema wameweka vizuizi ili kuwakabili hata wanaotumia gari au pikipiki kufanya uhalifu.
“Tumeweka vizuizi kwen ye barabara tatu kubwa ambazo zinatumiwa zaidi na vyombo vya usafiri kuingia na kutoka likiwamo Daraja la Mwananchi, na barabara inayotokea Kimara,” alisema mtendaji huyo.
Alisema wanaweka vizuizi kuanzia saa sita usiku na kila gari linaylotoka au kuingia mitaa hiyo linakaguliwa.
Mjumbe wa Mtaa wa Twiga, Mohammed Kalega alisema baada ya kuanza kuongezeka kwa matukio ya uhalifu wamebadilisha mfumo wa kulinda kwani ulinzi shirikishi sasa ni saa 24, wapeana shifiti.
“Kuna wanaoingia asubuhi hadi saa mbili usiku na wengine wanaingia usiku hadi asubuhi. Tunafanya hivyo kuhakikisha mtaa unakuwa na usalama wa kutosha kwa watu wote,” alisema.
Imeandikwa na Elizabeth Edward, Aurea Simtowe na Tuzo Mapunda.