Makamba akumbushia misukosuko waliyopitia na Kinana, ataka awasamehe wote

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba amemuomba Makamu Mwenyekiti wa CCM aliyechaguliwa Abdulrahman Kinana kusahau yaliyopita na kusamehe.



Dodoma. Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba amemuomba Makamu Mwenyekiti wa CCM aliyechaguliwa Abdulrahman Kinana kusahau yaliyopita na kusamehe.

Makamba amesema kuwa yeye na Kinana waliwahi kunyeshewa mvua kwa kuitwa kwenye kamati ya maadili na yaliwakuta huko.

Amesema kiongozi mwenye busara na hekima huwa anasamehe hivyo angetamani kuona kiongozi huyo akiwasamehe waliokuwa wamewashughulikia ambao baadhi amesema wapo kwenye mkutano.

"Leo yameisha, wewe ndiyo bosi wao hivyo nenda ukawaongoze, jenga tabia ya kusamehe na kuwasamehe maana na wengine wapo hapa," amesema Makamba.

Kinana na Makamba waliwahi kuitwa kwenye kamati ya maadili ya CCM chini uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, John Magufuli na Katibu Mkuu, Dk Bashiru Ali.

Kamati hiyo ilikuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula ambaye jana aliandika barua ya kung'atuka ndipo nafasi yake ikachukuliwa na Kinana.