Makamba awatuliza wabunge wanaorushiana makombora

Makamba awatuliza wabunge wanaorushiana makombora

Muktasari:

  • Mbunge wa Bumbuli (CCM),  January Makamba amewataka wabunge wanaotoa maoni na ushauri wenye nia njema wasibezwe  wala kuhukumiwa.

Dodoma. Mbunge wa Bumbuli (CCM),  January Makamba amewataka wabunge wanaotoa maoni na ushauri wenye nia njema wasibezwe  wala kuhukumiwa.

Makamba ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 14, 2021 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kwa sasa nchi inahitaji umoja na utulivu na kwamba kauli za utengano, kutiliana shaka, kutuhumiana na kuhukumiana hazijengi bali zinawachanganya Watanzania akibainisha kuwa mambo makubwa aliyoyafanya rais wa awamu ya tano, Hayati  John Magufuli hayatafutika, hayafutwi, hayatapotea na hayatapotezwa kwa kauli yoyote ile ya kubeza.

“Dhamira ya kauli na ushauri na maoni iko ndani ya moyo wa mtu. Atakaposifu kwamba mama Samia (Rais Suluhu Hassan) ameanza vizuri, asihukumiwe kuwa anatafuta cheo. Anapokosoa asionekane kuwa ananongwa, anapokaa kimya isiwe kwamba amesusa. Naomba sana tusihukumiane katika dhamira za kauli,” amesema.

Amesema kazi aliyoifanya Rais Magufuli anaweza kuichukulia kama fundi aliyeshona nguo nzuri na akitokea mtu akaona kwenye  nguo kuna uzi umejitokeza isionekane kuwa ni dhambi.

“Akatokea mtu akasema kwenye hii nguo kifungo kimelegea hebu tukiweke vizuri isionekane kuwa huyu mtu ni msaliti. Na mtu huyo anapokaza kifungo nguo ikapendeza bado sifa ni ya mshonaji,” amesema.

Makamba atema cheche bungeni | Mambo makubwa aliyofanya Magufuli hayatafutika || Watu wasibezwe

Makamba amebainisha kuwa ametoa kauli hiyo kwa sababu dalili alizoziona sio nzuri na viongozi wanayo haki na wajibu wa kutoa maoni kuhusu mambo yanavyopaswa kwenda.

“Lakini njama, vikundi na vigenge vya kuweka mashinikizo kwamba kipi kifanyike, hatua zipi zichukuliwe si sawa kabisa na haitujengei umoja,  uongozi wa nchi ni jukumu kubwa na la kihistoria,” amesema.

Amesema  Rais  wa nchi ana madaraka na nguvu kubwa na kwa vyovyote vile katika uongozi wake anaacha alama.

Katika uchambuzi wa utendaji wa marais, Makamba amesema rais wa awamu ya kwanza, Hayati Julius Nyerere na waliofuatia hadi Magufuli wameacha alama na ndio asili ya jukumu  kulinda yote ambayo viongozi wameyafanya.

“Sisi tupiganie yaliyofanywa na Magufuli lakini tusipigane, wakipigania mambo ya nyuma watashindwa kupigania mambo ya mbele ambayo rais mpya anatakiwa kuyafanya,” amesema.