Makamba: China  inaongoza kwa ukubwa wa biashara kati yake na Tanzania

Muktasari:

  • Waziri Makamba -Uhusiano kati ya taifa la China na Tanzania umeleta tija kubwa ikiwemo kuchochea ukuajia wa biashara na uwekezaji nchini.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema mahusiano kati ya  Tanzania na China  yamekuwa na manufaa makubwa ikiwemo  eneo la biashara na uwekezaji.

Hayo ameyabainisha leo Septemba 26, 2023 akiwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya sherehe ya kusherekea miaka 74 tangu kuanzishwa kwa Taifa la watu wa Jamuhuri ya China iliyofanyika katika ofisi za ubalozi huo.

Katika maelezo yake Waziri Makamba amesema sekta hiyo imekuwa ikikua kwa kasi na China imekuwa moja kati ya nchi inayoongoza kwa kuleta mitaji mingi nchini.

"China  inaongoza kwa ukubwa wa biashara kati yake na Tanzania na imekuwa ikipanda katika sekta ya utalii, tunajivunia mahusiano yetu yaliyodumu kwa miaka 60 sasa na kadri miaka inavyoongezeka ushirikiano wetu umekuwa," amesema 

Amesema  hata Rais Samia Suluhu Hassan alipewa heshima ya kutembelea China Mwaka jana kufanya ziara ya kitaifa na katika safari hiyo viongozi  wote waliweza kusisitiza namna ya kuwa karibu.

Awali, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Richard Kasesela amesema ndani ya kipindi hicho chama hicho kimepata manufaa makubwa kwenye kuwanoa viongozi wake mafunzo ya uongozi.

"Sisi na chama tuna timiza miaka 59 ya diplomasia  kati ya Tanzania na China na tunajivunia viongozi wengi wamepata mafunzo ya uongozi kutoka kwao.

"Kwetu ni sherehe na tunatimiza miaka 59 tunajivunia viongozi wetu wengi wamepitia  mafunzo ya uongozi  na tumepewa na  China tunajivunia," amesema 

Kwa upande wake Balozi wa China, nchini Tanzania Chen Mingjian, amesema ushirikiano wa taifa hilo  na Tanzania ni wakihistoria na bado wako mstari wa mbele kuunga mkono maendeleo.

"Kupitia sherehe kama hii bado tunaendelea kudumisha ukaribu wetu uliohenziwa na viongozi wa mataifa yetu mawili na kuendelea kuwa kitu kimoja, katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo " amesema

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye na Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu