Makonda aja na miradi mipya 57 Dar

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mwaka 2020 miradi mipya 57 itatekelezwa katika mkoa huo lengo likiwa ni kuwasogezea huduma wananchi.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mwaka 2020 miradi mipya 57 itatekelezwa katika mkoa huo lengo likiwa ni kuwasogezea huduma wananchi.

Makonda ameeleza hayo leo Jumatano Januari 15, 2020 katika uzinduzi wa mfumo wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa huo.

“Zawadi zitaendelea kwa wananchi na ndio  maana nasema hiyo miradi 57 inakuja kwa ajili ya wakazi wa Dar es Salaam,” amesema Makonda.

Mwananchi lilipotaka kujua miradi hiyo ni ipi,  Makonda amesema ni iliyopo katika ilani ya uchaguzi wa CCM lakini bado haijatekelezwa na  mingine ni mipya kabisa.

Kuhusu mfumo huo,  Makonda amesema unalenga kutatua changamoto ya kusuasua kwa miradi, kwamba teknolojia itatumika kukusanya taarifa na kuzitumia kurahisisha kazi.

“Niwaombe watu wa Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) wazidi kuwa wabunifu kuja na mifumo ya namna hii inayowezesha kukusanya taarifa na hata kufuatilia kwa njia ya mtandao,” amesema Makonda.