Makonda anapambana na nani?

atibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda.

Moshi/Dar. Staili ya utendaji kazi wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda kuwananga makada wenzake, watendaji serikalini, wakiwamo mawaziri na vyama vya upinzani, inaibua swali lisilo na majibu kuwa anapambana na nani hasa?

Kwa utamaduni uliozoeleka wa siasa za Tanzania, ilitarajiwa katika kukiimarisha chama hicho tawala, Makonda angeelekeza mashambulizi yake kwa vyama vya upinzani pekee, hususani chama kikuu cha upinzani, Chadema, lakini staili yake ni tofauti.

Ingawa wengine wanamuona kama anaivua nguo CCM na Serikali yake kupitia mikutano yake ya hadhara, baadhi ya wachambuzi wa siasa nchini wanaona kama staili ya Makonda ya kutatua kero papo hapo, inakiimarisha chama hicho.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Kristomus Faraja, alienda mbali na kueleza anachofanya Makonda ni kujaribu kukitenga chama chake na matatizo wanayopitia wananchi, ili kuwaaminisha chama kinaisimamia Serikali yake.

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza yeye alienda mbali na kueleza Makonda ni zaidi ya Katibu mwenezi, hajapata kutokea wa aina yake, akitaja faida za ujio wa Makonda.

“Sasa tunajua hali yetu si njema. Hakuna utawala wa sheria wala wa mfumo. Sasa tunajua hasara za kukaa gizani. Ukikosa upinzani bungeni na mabarazani, ukakosa uhuru wa habari, ukakosa wanaharakati huru, unastawisha chawa kila mahali.”

“Sasa tunajua wananchi wanaona bora dikteta kuliko demokrasia, yaani bora shibe ya gerezani kuliko njaa ya uraiani. Sasa tunajua wenye shida wanataka mtu si taasisi wala mfumo. Sasa tunajua kila suluhisho linazaa tatizo.”

“Sasa tunajua hakuna Bunge huru, hakuna mahakama huru, hakuna DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini) huru, hakuna AG (mwanasheria mkuu wa Serikali) huru, ila kuna chama huru,” ameeleza Bagonza katika andiko linalosambaa mitandaoni na ambalo amethibitisha ni la kwake.

Makonda mwenyewe hakupatikana kuzungumzia namna staili yake inavyochanganya wengi, kiasi cha watu kushindwa kuelewa adui yake hasa ni nani katika ziara zake, licha ya yeye kwenye mikutano amekuwa akisema: ‘Nitasema ukweli hata kama watu hawataupenda.’

Hata hivyo, baadhi wanaona staili ya Makonda haitofautiani sana na iliyotumiwa na Nape Nnauye alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kati ya mwaka 2012 na 2015, ambapo alizunguka nchi nzima na kuzungumza na wananchi.

Kipindi hicho, Nape na aliyekuwa Katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye sasa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, walijiwekea utaratibu wa kufanya ziara mikoani na kusikiliza kero za wananchi na kuimarisha uhai wa CCM.

Katika ziara hizo, kama ilivyo sasa ziara za Makonda, baadhi ya wananchi walilalamikia baadhi ya watendaji wa Serikali kushindwa kutatua kero zao, wakiwamo mawaziri na huko ndipo lilipoasisiwa neno “mawaziri mizigo.”

Nape aliwahi kukaririwa akisema, “CCM kama ilivyo agizo la mkutano mkuu (wa CCM) la kuwasemea wananchi, tulisikiliza kilio chao na kwa kufuata utaratibu, baadhi ya mawaziri waliitwa na kuhojiwa na kamati kuu Desemba 2013.”

Tofauti na Nape na Kinana ambao katika mikutano hiyo walikuwa hawawashurutishi watendaji kujibu malalamiko ya wananchi hadharani, Makonda yeye amejenga utamaduni wa kutaka utatuzi wa papo kwa hapo wa kero za wananchi.

Lakini tangu ateuliwe na Halmashauri Kuu ya CCM baada ya jina lake kupendekezwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu kushika wadhifa huo Oktoba 2023, na kuzunguka mikoani akifanya mikutano ya hadhara, Makonda ameingia katika misuguano ndani ya CCM, serikalini na hata nje ya vyombo hivyo.

Utendaji wake huo unaonekana kumfanya atengeneze maadui ndani ya CCM na Serikali inayoongozwa na CCM, huku baadhi ya wachambuzi wakiona ziara zake hazikijengi chama hicho, bali zinakivua nguo kuwa mifumo ya Serikali inapwaya.

Kauli za hivi karibuni za Makonda mwenyewe zinathibitisha kuwa kuna moto unaowaka chini kwa chini ambapo akiwa Rukwa, aliwaambia viongozi na watendaji wa Serikali, wakiwamo mawaziri kuwa sio lazima wampende.

“Tutaweka bayana udhaifu wa kila sekta ili mtu ajitathmini, anafanya kazi yake kama inavyotakiwa? Hatuwezi kuwa tunalipwa mshahara halafu wengine hamfanyi kazi,” alisema Makonda na kuahidi kukabidhi ripoti kwa Rais.

“Bahati mbaya wengine wamepewa wizara badala ya kuhangaika kufanya kazi ya wizara ili kujenga heshima ya Rais, wanahangaika kutengeneza mitandao yao kuwalipa watu kuwasifia wakati kwenye mamlaka yao mambo hayaendi vizuri,” alisema.

Kauli nyingine inayothibitisha kujijengea uadui ndani na nje ya Serikali, ni pale aliposema kwa kuwa amepewa usemaji basi atasema kweli bila kumung’unya maneno, na hatakufa na Mungu hana mpango wa kumuondoa kwanza.

“Mtege sumu kwenye vyumba mnapoteza muda tu, mtafute waganga mnapoteza muda tu. Nataka kila kiongozi awajibike kwenye nafasi yake,” alisema na kuonya dawa inachemka kwa wanaosubiri ziara za Rais kisha wamsifie anaupiga mwingi.

Lakini Januari mwaka huu, Makonda alimvaa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akimtaka aache kuendeleza kile alichodai ni tabia ya upotoshaji kama kete yake kubwa ya kufanya siasa, na kumtweza Rais na kuwadhalilisha Watanzania.

Kauli hii aliitoa saa chache baada ya Mbowe kutangaza chama chake kuandaa maandamano ya amani na kueleza kwa kirefu maridhiano yaliyokuwa yakiendelea baina ya chama tawala na Chadema, ni kama yamevunjika rasmi.

Mashambulizi kama hayo aliyatoa juzi akiwa mkoani Mbeya alipowataka Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Tundu Lissu na wenzake, “kuacha kulialia na badala yake  waingie ‘site’ ili kufanya siasa, kwani wamemuacha anatamba mwenyewe.”


Mitazamo tofauti ya wanazuoni

Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Revocatus Kabobe, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mhadhiri katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) amesema ziara hizo za Makonda zina manufaa si tu kwa wananchi, bali kwa CCM na Serikali yake.

“Vita ya Makonda inalenga kukiongezea chama chake kura na kuaminiwa zaidi kwamba bado kiko hai. Anaeneza itikadi ya chama chake kwa wananchi na huwezi kutenganisha itikadi ya chama na matatizo ya watu,” amesema Dk Kabobe.

Hata hivyo, amesema anachokifanya Makonda si namna sahihi ya kutatua changamoto za wananchi, isipokuwa inapaswa kuwekwa mifumo bora kwenye taasisi ambayo haitahitaji mwenezi kutembelea kila eneo la nchi.

“Hii nchi ni kubwa, hakuna kiongozi anayeweza kufika kila kona ya nchi. Tuwe na mifumo imara ya kufanya kazi, ikisimama humhitaji Makonda au mkuu wa wilaya kwa sababu tutakuwa na mifumo bora ya usimamizi kuanzia chini,”amesema.

Pia amesema, Makonda anapambana na upinzani ambao wamekuwa wakifanya mikutano ya hadhara tangu kuondolewa kwa zuio la mikutano ya vyama vya siasa.

Mhadhiri huyo amesisitiza: “Chama ni watu, na watu wanasikiliza chama kimesema nini. Makonda anapopita anaamsha watu kwamba jamani, CCM bado ipo.”

“Chadema wamekuwa wakifanya mikutano yao maeneo mbalimbali, hivyo mikutano ya Makonda ni kujaribu kufuta kile kilichofanywa na Chadema na kuwaaminisha watu kwamba CCM bado kinafanya kazi,” ameongeza kusema.

Ameeleza kumekuwa na tafsiri kwa baadhi ya watu kumtafsiri kama mtu anayetoa maagizo binafsi kwa watendaji wa Serikali wakiwemo mawaziri, akisema Makonda anakiwakilisha chama na anachokifanya ni kazi ya chama na sio yake.

Dk Kristomus Faraja, Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema mikutano anayoifanya Makonda ni faida kwa chama, kwani inatengeneza uhalali wa chama chake kwa wananchi.

“Anachojaribu kuonyesha wananchi ni kukitenga chama na matatizo wanayopitia. Anawafanya wananchi waone kwamba chama kinaiwajibisha Serikali, kinataka wananchi wasihusishe shida zao na chama,” amesema.

Amesema licha ya mfumo wa utatuzi wa matatizo anaoutumia Makonda kutokuwa bora, anachokifanya ni kueneza itikadi za chama kama mwenezi.

Pia amesema vyama vya upinzani vinapaswa kujipanga na kujibu mashambulizi ambayo yamekuwa yakielekezwa dhidi yao na mwenezi huyo, kupitia mikutano ya hadhara ambayo kila chama kimeruhusiwa.

“Nafasi ipo ya kila chama kutoka na kueleza wananchi sera zao. Wanapaswa kuitumia nafasi hiyo na sio kulalamika,” ameongeza Dk Faraja akihojiwa na gazeti hili.