Makongoro aeleza mapokeo yake Mwalimu Nyerere alipotaka kung’atuka

Mtoto wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere akizungumza kwenye mdahalo wa kitaifa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere unaofanyika katika Shule ya Uongozi Kibaha mkoani Pwani leo Jumamosi Aprili 9, 2022.

Muktasari:

Mtoto wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, ameeleza namna baba yake alivyomshirikisha nia ya kutaka kunga’atuka kwake mwaka 1980 na wasiwasi aliokuwa nao.

Dar es Salaam. Mtoto wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere ameeleza namna baba yake alivyomshirikisha nia ya kutaka kung’atuka mwaka 1980 na wasiwasi aliokuwa nao.

🔴 #LIVE: MDAHALO WA KITAIFA KUADHIMISHA MIAKA 100 YA KUZALIWA MWALIMU NYERERE

Makongoro ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, ameyasema hayo leo Jumamosi Aprili 9, 2022 kwenye mdahalo wa kitaifa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere unaofanyika katika Shule ya Uongozi Kibaha mkoani Pwani.

Makongoro aliyekuwa akiwakilisha familia ya Hayati Nyerere katika mdahalo huo, amesema kabla ya kung’atuka, Mwalimu Nyerere alimshirikisha nia ya kufanya hivyo na akaelewa hoja zake zilikuwa na mashiko.

Amesema moja ya jambo ambalo alimpinga wakati akimuwasilishia hoja zake hizo za kung’atuka ni kuwa ataishije bila kuwa mtoto wa Rais.

“Hoja zote nilimuelewa Mwalimu Nyerere, lakini wasiwasi wangu ilikuwa nimeshazoea kuishi kama mtoto wa Rais, sasa itakuwaje akiondoka, ina maana nitaishi kama mtoto wa Mwalimu na sio Rais,”amesema Makongoro.

“Pamoja na yote yaliyotokea ya Mwalimu kung’atuka na baadaye kufariki, nashukuru mpaka sasa ninaishi kama mtoto wa Mwalimu, na nimekuwa nikifanya mambo mengi kwa ajili ya jina lake na hata leo nipo hapa kwa ajili yake yeye.

“Kwani ukitafuta mambo ambayo Makongoro amewahi kufanya katika nchi hii, unaweza ukatafuta mpaka ukome, lakini nipo kwa ajili ya Mwalimu, ni kupitia jina lake, nimeweza kusafiri nchi mbalimbali, ikiwemo Afrika Kusini na Namibia kuchukua tuzo ya Mwalimu Nyerere, maeneo ambayo nilikuwa sijawahi kwenda” amesema Makongoro ambaye ni mtoto wa tano wa Hayati Nyerere.

Amesema kupitia matukio hayo mbalimbali, Mwalimu Nyerere amekuwa akizidi kumshangaza kila siku licha ya kuwa hayupo duniani.

Makongoro amesema Mwalimu Nyerere alipenda sana suala la ubinadamu na alikuwa na maono ya mbali ambayo baadhi aliyaona na mengine hakufanikiwa kuyaona ikiwemo ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere na Serikali kuhamia Dodoma.