Malasusa: Wakati mwingine kuikemea dhambi kunaweza kukupunguzia marafiki
Dar es Salaam. Waumini wa dini ya Kikristo nchini wamekumbushwa kuishi maisha aliyoishi kiongozi huyo ikiwemo kutenda mema na kujiepusha na dhambi.
Kauli hiyo imetolewa leo, April 9, 2023 na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa wakati akiongoza ibada ya Pasaka, iliyofanyika Azani Front.
Mbali na kujitenga na dhambi, Askofu Malasusa amewataka wazazi kuwafundisha watoto na vijana wao, malezi bora na maadili mema ili kuepuka mmomonyoko wa maadili.
Amesema kukosekana kwa maadili katika familia kumesababisha kuwepo kwa baadhi ya vijana ambao hawana maadili katika jamii.
"Ndugu zangu kukemea dhambi huwa kuna gharimu na wakati mwingine kuikemea dhambi kunaweza kukupunguzia marafiki, lakini dhambi zako wewe mkristo ni lazima uzikemee.
"Yesu katika mafundisho yake, anasema mtu aliyeishi katika dhambi anamlinganisha na maiti, hivyo mtu anapomrudia Yesu anakuwa amefufuka.
"Yesu anatamani siku kama ya leo, kila mmoja kuanza maisha mapya ya kufufuka pamoja na yeye na kuacha dhambi.
"Kristo ametupa ufahamu wa kutambua mema na mabaya lakini pia ametupa ujasiri wa kukemea dhambi na kujua yale yasiyompendeza Mungu, hivyo tunaposhangilia ufufuo, tunapofurahi ufufuo wake tuziache dhambi, tusishikamane na dhambi tena tusiendelee na matendo yanayomhuzunisha Mwenyezi Mungu" anabainisha Askofu Malasusa.