Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama alivyoficha sare za shule za bintiye ili akatishe masomo

Mtoto Sikujua Dickson (16) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadogo zake na mama yake mzazi, Pili Dickson (55) wakazi wa mtaa wa Itagano Jijini Mbeya. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Wakati Serikali na asasi mbalimbali za kiraia zikifanya jitihada za kusomesha watoto wa kike, hali imekuwa tofauti kwa mwanamke huyo aliyekuwa kikwazo kwa mtoto wake mwenyewe, jambo linalopingwa na jamii.

Mbeya. Katika hali isiyo ya kawaida, mama mmoja amebainika kuwa kikwazo kwa mtoto wake wa kike kuendelea na masomo baada ya kuficha sare zake za shule, kwa lengo la kumzuia kuendelea na masomo ya sekondari.

Mama huyo, Pili Dickson (55) anadaiwa kumfanyia vitendo vya kikatili mtoto huyo, Sikujua Dickson (16), mwanafunzi wa kidato cha pili, jambo ambalo limeibuliwa na wananchi katika kata ya Itagano jijini Mbeya, anapoishi mwanamke huyo na familia yake.

Wakati Serikali na asasi mbalimbali za kiraia zikifanya jitihada za kusomesha watoto wa kike, hali imekuwa tofauti kwa mwanamke huyo aliyekuwa kikwazo kwa mtoto wake mwenyewe, jambo linalopingwa na jamii.

Wananchi wa kata ya Itagano wamepasa sauti zao kuitaka Serikali kuingilia kati suala hilo ili kunusuru ndoto za mtoto huyo ambaye ameonyesha nia ya kutaka kuendelea na masomo yake licha ya changamoto anazopitia.

Mtoto huyo anasoma shule ya sekondari Itagano huku ikielezwa kwamba mbali na sare zake za shule kufichwa, mama yake amekuwa akimfanyia vitendo vya kikatili kama kupigwa, kutukanwa, kunyimwa chakula na hata kuzuiwa kujisomea nyumbani.

Hali hiyo inadaiwa kumuathiri mtoto huyo kisaikolijia kwa kiwango kikubwa na kusababisha ashindwe kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto yake ya kupata elimu.

Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano nyumbani kwao, Sikujua amesema endapo atakosa msaada kwa kutenganishwa na mama yake, ndoto yake ya kupata elimu na kuja kuwa daktari itapotea.

“Sisi tumezaliwa watatu, baba alifariki  tumeishi maisha ya mateso kwa sababu mama akitoka kulewa anatupiga na hata kutunyima mahitaji muhimu kama chakula, maradhi na hata nikiwa hedhi nashindwa kujisitiri,” amesema.

Ameongeza: “Maisha ninayopitia ni magumu, nalala chini na wadogo zangu, hata nikitaka kujisomea mama ananinyang’anya madaftari na kunipiga, anasema nikisoma napata faida gani,” amesimulia mtoto huyo.

Sikujua amesema maisha hayo yanaondoa mwanga wa kufikia ndoto zake na kuwasaidia wadogo zake ambao pia wanapitia changamoto hizo.

Sikujua amesema kuwa ili kufikia malengo yake, amemuomba mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kupitia taasisi yake ya Tulia Trust, kuisaidia familia yake akiwemo yeye kwa kumtenganisha na mama yake na kumsaidia mahitaji muhimu ya elimu.

“Namuomba Dk Tulia popote alipo anisaidie, aokoe familia yetu kutoka kwenye manyanyaso, mateso, vipigo na kukosa haki ya kupata elimu,” amesema Sikujua.

Hata hivyo, alipohojiwa kuhusu madai ya mwanawe, mwanamke huyo, Pili Dickson amekiri makosa hayo huku akieleza kwamba ugumu wa maisha ndiyo umesababisha kuwatendea hivyo.

“Naomba mnisaidie, naishi maisha magumu, nimejaliwa kupata watoto watatu, wawili wanasoma, mmoja ameshindwa kuanza masomo kutokana na uchumi duni,” amesema mwanamke huyo huku akikiri kuficha sare za mtoto wake ili ache shule kutokana na ugumu wa maisha.

Akizungumzia maisha ya familia hiyo, mjumbe wa shina, Exsalina Frank amesema watoto hao wanaishi mazingira magumu kuanzia kula, kulala na mahitaji mengine muhimu na amemuita mara kadhaa kumkanya kuhusu tabia.

“Kama mlivyoona ndani hali ilivyo, watoto wameleta malalamiko mara kadhaa, mama yao akisaga unga anaficha ili wasipike na kula na hata mahitaji wakiomba anawaeleza wamfufue baba yao kaburini.

“Awali kabla ya baba yao kufariki, watoto walikuwa na maisha mazuri lakini baada ya kufariki wamekuwa wakiishi kwa mateso makubwa, wanapigwa mara kwa mara na kunyimwa haki za msingi za chakula, kulala na elimu,” amesema.

Diwani wa Kata ya Itagano, Yuda Sekabenga amekiri kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kuhusiana na maisha ya watoto hao kunyanyaswa kwa kupigwa, kunyimwa chakula na kuficha sare za mtoto wake kwa lengo la kumkatisha masomo.

Mwalimu wa taaluma katika shule anayosoma Sikujua, Pascal Mathias amesema licha ya mwanafunzi huyo kupitia changamoto za ukatili kutoka mama yake amekuwa mtiifu na kufanya vyema kwenye masomo.

Mathias amesema kwenye taaluma amekuwa akifanya vizuri ambapo katika mhula wa mitihani mwaka 2022, alishika nafasi ya 15 kati ya wanafunzi 34 huku kwa mwaka 2023 amepanda na kufikia nafasi ya tisa  katika idadi hiyo ya wanafunzi.

“Hayo yote yaliyosemwa ni kweli, hata hivi sasa kapunguza manyanyaso baada ya kumuita kwenye kikao ofisini kwa mtendaji wa mtaa na kumpa onyo lakini bado mazingira ya familia hiyo ni mabaya hata kiusalama tu,” amesema.

Kufuatilia malalamiko hayo, Taasisi ya Tulia Trust imefika kwenye makazi wanayoishi na kumkabidhi mwanafunzi huyo mahitaji muhimu ya shule kama sare za shule, viatu pamoja na kuutaka uongozi wa shule kumtafutia makazi salama ili apate elimu bora wakati wakiangalia namna ya kumpeleka shule ya bweni.

 “Inasikitisha sana, kama taasisi tumejitolea kumsomesha na kumpatia mahitaji yote na kuomba uongozi wa shule kumtafutia makazi salama ambayo yatalipiwa na Spika wa Bunge na mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson,” amesema Meneja wa Tulia Trust, Jackline Boaz.