Mama amuunguza mwanaye akimtuhumu kumchonganisha na mumewe

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka.

Muktasari:

  • Mama huyo aliyetengana na mumewe Aprili mwaka huu, anadaiwa kumfungia ndani mwanaye wa kumzaa na kuweka kisu kwenye moto na kilipopata moto akaanza kumchoma maeneo mbalimbali ya mwili na kumsababishia majeraha kiasi cha kulazwa katika hospitali ya Wilaya ya Siha.

Siha. Mkazi wa Kijiji cha Kilingi, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Jackline Kiwelu (42), anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa akituhumiwa kumuunguza kwa kisu chenye moto mwanaye wa miaka sita, sehemu mbalimbali za mwilini akimtuhumu kumchonganisha na mumewe waliyetengana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipoulizwa kuhusu tukio hilo, amesema analifuatilia.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi Digital jana Desemba 7, 2023 Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka amesema tukio hilo la kikatili lilitokea Desemba 4, mwaka huu baada ya mama huyo kumfungia ndani mwanaye na kuanza kumfanyia ukatili huo, uliomsababisha majeraha na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Siha anakopatiwa matibabu.

"Huyu mama ni kweli alimfanyia mwanaye wa kumzaa ukatili, kwa kumuunguza na kisu chenye moto sehemu mbalimbali za mwili wake, kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria," amesema Dk Timbuka.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo, mtoto huyo ambaye amelazwa hospitalini hapo (jina linahifadhiwa), ameeleza kuwa, siku hiyo mama yake alimwita ndani na kuweka kisu kwenye jiko na kilipopata moto alianza kumuunguza nacho sehemu za makalioni, mapajani na mdomoni huku akimuita mbea.

"Hiyo siku mama aliniita ndani akawa ameshika kisu mkononi na kukiweka kwenye moto na baada ya kushika moto akaanza kuniunguza na kuniambia mimi ni mbea natoa maneno na kumpekea baba yangu," ameeleza mtoto huyo.

Akizungumzia tukio hilo, baba mzazi wa mtoto huyo, Steven Shayo amesema taarifa kuhusu ukatili huo alizipata usiku wa Desemba 4, 2023 kutoka kwa majirani, wakimweleza unyama aliofanyiwa na mama yake mzazi, na ndipo alipofika nyumbani kumchukua mwanaye na kumpeleka hospitali.

Shayo ambaye ameachana na mke wake huyo, amesema tukio hilo limemhuzunisha kama mzazi na alichokifanya mwanamke huyo ni ukatili wa kinyama.

"Niliachana na mke wangu tangu Aprili mwaka huu, sasa juzi nilipopata taarifa za tukio hili ambalo kiukweli limeniumiza nilifika hapa nyumbani nikamkuta huyu mtoto yupo ndani pamoja na dada yake, nikawauliza ni kitu gani kimetokea.

"Nilimuuliza dada yake kuhusu tukio zima akasema mama alichukua kisu akakipasha kwenye moto na kuanza kumuunguza mtoto sehemu za mdomoni, mgongoni na sehemu nyingine na alifanya tukio hilo saa 2 usiku, akisema alichukua maneno kutoka kwa mama yake na kuyaleta kwangu ndio maana alimuadhibu," amesema.

Naye, Mwenyekiti wa Kitogoji cha kilingi Kati, Paul Padame amesema tukio hilo limemhuzunisha na kwamba ni la kikatili, hivyo akaitaka jamii kuacha kufanya matendo ya kinyama kwa watoto.