Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama asimulia furaha ya kupata pacha watano ilivyogeuka majonzi

Muktasari:

  • Watoto hao, waliozaliwa usiku wa kuamkia Julai 26, 2026, katika wiki ya 26 ya ujauzito, walikuwa wawili wa kiume na watatu wa kike.

Watoto hao, waliozaliwa usiku wa kuamkia Julai 26, 2026, katika wiki ya 26 ya ujauzito, walikuwa wawili wa kiume na watatu wa kike.

Bertha Ismail

Arusha. Kilichokuwa ndoto ya Robert Frank na mkewe, Careen Remi (22), ya kuupokea kwa furaha uzao wao wa kwanza wa watoto watano pacha, kimegeuka kuwa majonzi baada ya watoto hao wote kufariki dunia saa chache baada ya kuzaliwa njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru.

Watoto hao, waliozaliwa usiku wa kuamkia Julai 26, 2026, katika wiki ya 26 ya ujauzito, walikuwa wawili wa kiume na watatu wa kike.

Akizungumza kwa uchungu, mama wa pacha hao, Careen amesema tangu madaktari walipobaini kupitia kipimo cha ultrasound kuwa alikuwa amebeba ujauzito wa pacha watano, aliwekwa chini ya uangalizi maalumu na kuhudhuria kliniki kila Jumatatu kufuatilia maendeleo ya ujauzito wake.

“Madaktari walikuwa wakinifuatilia kwa karibu na kunipa matumaini kwamba ningejifungua salama, nilikuwa na moyo na matumaini na niliamua kufuata maelekezo yote niliyopewa na kila wiki nilikuwa nafika kliniki kwa uchunguzi,” amesema.

Amesema usiku wa Julai 25 alianza kupata maumivu makali ya tumbo na kuwahishwa hospitalini, ambako madaktari walibaini alikuwa ameanza uchungu wa kujifungua kabla ya wakati.

Amesema baada ya kubainika hivyo aliwahishwa chumba cha kujifungua na alifanikiwa kujifungua watoto wawili wa kwanza wakiwa hai na kupelekwa katika chumba cha uangalizi wa watoto wachanga, baadaye akajifungua wengine wawili wakiwa hai, huku mtoto wa tano akizaliwa akiwa tayari amefariki dunia.

“Hata baada ya mtoto wa tano kuzaliwa akiwa amefariki, nilikuwa na matumaini kwa wale wanne waliokuwa hai, nilishukuru Mungu kwa yote.”

“Lakini ilipofika asubuhi nikaanza kupewa taarifa kuwa wanangu walikuwa wanafariki mmoja baada ya mwingine hadi wote wakamalizika,” amesema kwa uchungu.

Amesema, “Nililia sana, lakini namuachia Mungu kila kitu na ninaamini atanijalia tena watoto.”

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru, Dk Kipapi Mlambo amesema watoto hao walizaliwa katika wiki ya 26 ya ujauzito, hatua ambayo huwafanya kuwa katika hatari kubwa kutokana na kutokamilika kwa ukuaji wa viungo muhimu vya mwili.

Amesema ujauzito wa watoto watano ulisababisha mama huyo kuanza uchungu kabla ya wakati kutokana na mfuko wa uzazi kulemewa na ukubwa wa ujauzito.

“Timu ya madaktari ilifanya kila juhudi kuhakikisha mama na watoto wanapata huduma stahiki. Kwa bahati mbaya, licha ya jitihada hizo, watoto wote walifariki dunia, huku mama akiendelea vizuri na hali yake ikiwa imara,” amesema.

Kwa upande wake, baba wa watoto hao, Robert Frank amesema familia imepokea msiba huo kwa uchungu mkubwa, lakini imeamua kumtegemea Mungu katika kipindi hiki kigumu.

Amesema wanajiandaa na taratibu za mazishi za watoto hao na eneo la kuzikia huku wakiomba Mungu kuwapatia nguvu na imani katika kipindi hiki kigumu.

“Ni maumivu ambayo ni vigumu kuyaelezea. Tulikuwa tunasubiri kwa hamu kuwapokea watoto wetu, lakini sasa tunajiandaa kuwapa heshima yao ya mwisho,” amesema.