Mama miaka mitano jela kwa kumdhuru mwanaye

Muktasari:

  • Mahakama ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro imemuhukumu  kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh300,000 Jackline Kilawe kwa kosa la kumuunguza mwanaye na kisu chenye moto sehemu mbalimbali za mwili wake.

Siha. Mahakama ya Wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro imemuhukumu  kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh300,000 mkazi wa kijiji cha kilingi, Jackline Kilawe (47) kwa kosa la kumfanyia ukatili  mwanaye wa miaka sita, kwa kumuunguza na kisu chenye moto sehemu mbalimbali za mwili wake.

 Mwanamke huyo alitiwa hatiani jana, Desemba 8, 2023 na Mahakama hiyo baada ya kukiri kutenda kosa hilo la ukatili dhidi ya mwanaye, ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Siha akiendelea na matibabu kutokana na majeraha aliyopata.

Mbele ya hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elibahati Petro, Mwendesha mashitaka wa Serikali, Kurwa Seni,  aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 4, mwaka huu kinyume na kifungu namba 169 A (1)(2)cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Baada ya mahakama hiyo kumtia hatiani mwanamke huyo alilipa faini ya Sh300,000 na kuachiwa huru.

Hata hivyo baada ya hukumu hiyo, mwendesha mashtaka alisema Serikali inakusudia kukata rufaa kupinga adhabu iliyotolewa na mahakama hiyo dhidi ya mwanamke huyo, kutokana na kitendo alichotendewa mtoto huyo.

Mtoto huyo ambaye amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Siha, alipohojiwa na gazeti hili,  alieleza kuwa siku ya tukio mama yake alimuita ndani na kuweka kisu kwenye jiko na kilipopata moto alianza kumuunguza nacho sehemu za makalioni, mapajani na mdomoni huku akimuita mbea.

"Hiyo siku mama aliniita ndani akawa ameshika kisu mkononi na kukiweka kwenye moto na baada ya kisu kushika moto akaanza kuniunguza na kuniambia mimi ni mbea natoa maneno na kumpekea baba yangu,"ameeleza mtoto huyo.