Mama mzazi amtaja ‘baba’ wa Diamond Platnumz

Mama mzazi amtaja ‘baba’ wa Diamond Platnumz

Muktasari:

  • Sanura Kassim maarufu mama Dangote ambaye ni mama mzazi wa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz amesema baba halisi wa mwanaye ni Salum Iddi Nyange na si Abdul Juma ambaye kwa miaka mingi amekuwa akifahamika kama baba wa mkali huyo wa Bongofleva.

Dar es Salaam. Sanura Kassim maarufu mama Dangote ambaye ni mama mzazi wa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz amesema baba halisi wa mwanaye ni Salum Iddi Nyange na si Abdul Juma ambaye kwa miaka mingi amekuwa akifahamika kama baba wa mkali huyo wa Bongofleva.

Mama Dangote ameeleza hayo leo Ijumaa Januari 15, 2021 baada ya kupigiwa simu na Dida, mtangazaji wa kipindi cha Mashamsham kinachorushwa na redio ya Wasafi kueleza kuhusu uhusiano kati ya Diamond na Ricardo Momo aliyekuwa akihojiwa na redio hiyo.

Katika majibu yake, mama Dangote amesema Ricardo na Diamond ni ndugu na baba yao ni Nyange ambaye kwa sasa ni marehemu.

Mama mzazi amtaja ‘baba’ wa Diamond Platnumz

Akizungumza na Mwananchi Digital baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo, Abdul amesema amefurahi kusikia jambo hilo akidai kuwa hata yeye alikuwa hajielewi wala kujitambua.

“Nadhani mhusika ameshazungumza sawasawa kabisa,” amesema Abdul na alipoulizwa sababu za kutoweka wazi jambo hilo amesema, “si mmeshapata jibu kwa mwenyewe mnataka mimi niseme nini tena wakati yeye ndio aliyebeba mimba.”

Amesema kuanzia leo amekubali kuwa Diamond si mwanaye na kuongeza kuwa huenda ndio sababu msanii huyo alikuwa hamsaidii chochote, “nimembeba tangu anatoka hospitali, tukamlea na tukagombana alipokuwa kidato cha kwanza sijawahi kusikia hayo.”