Mama, wanawe watatu wafariki baada ya nyumba waliyolala kuungua moto

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo

Muktasari:

  • Watu wanne akiwemo mwanamke mmoja na watoto wake watatu katika kijiji cha Chidede Kata ya Luagala wilayani Tandahimba, wamefariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuungua moto usiku wa Juni 21 mkoani Mtwara.

Mtwara. Watu wanne akiwemo mwanamke mmoja na watoto wake watatu katika kijiji cha Chidede Kata ya Luagala wilayani Tandahimba, wamefariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuungua moto usiku wa Juni 21 mkoani Mtwara.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital leo Juni 22, 2023 shuhuda wa tukio hilo, Saidi Hassan (30) amesema tukio hilo limetokea saa 4 usiku wa kuamkia Juni 21, 2023 kwa nyumba ya, Rehema Nyapala kuungua moto na kusababisha vifo vya watoto watatu kufariki dunia papo hapo na mmiliki wa nyumba hiyo akiokolewa kutoka ndani.

Saidi amesema yeye alikuwa anatokea katika banda la video baada ya mmoja wao walikuwa katika banda hilo kutoka nje na kuona nyumba ikiungua moto na kutoa taarifa kwa watu wote waliokuwemo katika banda hilo.

“Tulikuwa tunaangalia picha katika banda la video, mmoja wetu alitoka nje na kuona moto na kutuambia kuwa kuna nyumba inaungua moto nikatoka nje na kuelekea kwenye eneo la tukio na nilipofika pale niliona mlango umefungwa kwa nje na nilitafuta mti na kupata mchi wa kinu na kubomoa mlango huku tukiita kumuita aliyeko ndani aje mlangoni ili tumuokoe.” amesema Saidi.

Saidi aliongeza kwa kusema kuwa baada ya kubomoa mlango alifika Khadija Mshamu Likundende ambaye alimtoa, Rehemu Nyapala akiwa ameungua vibaya na moto katika mwili wake na kumtoa nje huku watoto wakishindwa kuwaokoa kwa sababu moto kuwa mkali na walikuwa tayari wamepoteza maisha wakiwa katika vitanda vyao.

Salum Seif Mpenda amesema saa 5 kasoro usiku alisikia vilio na alipofika eneo la tukio aliona, Rehema Nyapala akiwa amelala chini ambapo alikimbizwa kwa kupelekwa kituo cha afya Luagala ambapo nao walimpa rufaa kwenda hospitali ya Nyangao na asubuhi ya leo Alhamisi walipokea taarifa kuwa, Rehema Nyapala amefarikia dunia.

kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara Nicodemus Katembo amesema kuwa Juni 21 saa nne usiku katika kijiji cha Chidede Rehema Hamisi (40) mkazi wa kijiji hicho akiwa ammelala nyumbani kwake na wanae wawili ambao ni Adhiru Shaha Bakari (12) mwafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Chidede, Imran Shadhili (3) na Muba Jafari Salum (15) ambaye ni mtoto wa dada yake, wakiwa wamelala usiku, nyumba yao ilishika moto na kuuungua na kusababisha vifo vya watu watatu katika eneo hilo la tukio.

“Mmoja wao Rehema Hamis aliokolewa na kukimbizwa hospitalini, hata hivyo; alifariki kabla njiani kabla ya kufika hospitali, chanzo cha tukio ni moto uliokuwa umewashwa ndani ya nyumba hiyo kwaajili ya kupikia ambao uliachwa bila kuuzima na baadae ukashika na kuunguza nyumba hiyo,” amesema RPC Katembo na kuongeza kuwa;

“Daktari amefanya uchunguzi wa miili ya marehemu na kubaini kuwa chanzo cha vifo vya marehemu ni kukosa hewa na kuungua sehemu kubwa ya miiili yao, marehemu hao wamekabidhiwa  kwa ndugu zao kwaajili ya maziko.”