Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo haya mwiba kwa waajiri  kuwatekelezea dada wa kazi

Muktasari:

  • Haitakupa shida kumtofautisha mfanyakazi wa nyumbani ‘Dada wa kazi’ na wanafamilia katika nyumba moja. Hii inatokana na namna waajiri wengi wanavyoishi nao.

Dar es Salaam. Kama ulidhani mfanyakazi wa nyumbani ‘house girl’ ni kiumbe anayestahili majukumu makubwa bila haki, unakosea, kwani  sheria inamlinda.

Hii inatokana na uhalisia kwamba, waajiri wengi wa wafanyakazi wa nyumbani, huwatumikisha kazi bila kufuata utaratibu na aghalabu ni kazi inayoonekana ya kudharaulika.

Kwa taarifa yako, haki aliyonayo mtumishi wa umma na mfanyakazi wa taasisi yoyote, ndiyo aliyonayo mfanyakazi wa nyumbani, kulingana na mkataba namba 189 unaolenga kukuza kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani.

Katika mkataba huo ambao Tanzania ipo mbioni kuuridhia, vipo vipengele vinavyoonekana kuwapa wakati mgumu waajiri kuvitekeleza, kutokana na mazoea waliyonayo juu ya kuishi na wafanyakazi hao.

Miongoni mwa vipengele hivyo ni haki ya faragha kwa mfanyakazi huyo, inayohusika kupewa chumba chake. Lakini uhalisia wafanyakazi hawa hulazwa na vijana wa waajiri au wakati mwingine sebuleni na koridoni.

Kipengele hicho kinamuibua aliyewahi kuwa mwajiri wa mfanyakazi wa nyumbani, Mary Elia anayesema vipato duni vinawasababisha kushindwa kumudu kupanga zaidi ya chumba kimoja au viwili.

“Hivyo kwa hali hii, ni wazi kwamba msichana atalala tu na watoto hamna namna  kwani kama una vyumba viwili , kimoja utalala na mume wako na kama hauna mume basi utalala na mtoto au watoto wako.

“Kile kinachobaki ambacho mara nyingi ndio hutumika kama jiko au sebule, ndipo atalala dada,” anasema Marry.

Wakati hali ikiwa hivi, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Jiji la Dar es Salaam, Joyce Maketa anasema ni hatari sana kuwalaza watoto na dada, kwa kuwa wote wamelelewa katika namna tofauti.

“Tumekuwa tukishuhudia baadhi ya kesi za wafanyakazi wa majumbani wakiwafanyia vitu vibaya watoto wa matajiri wao ikiwemo mambo ya kishirikina, kuwalazimisha kufanya nao ngono bila kujali umri wao na mwishowe kuwaambukiza magonjwa ya zinaa, hivyo ni vema dada akawa na chumba chake sio kwa usalama wake tu bali na  watoto wako pia,”alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi majumbani, Zanini Othuman anasema kumlaza mfanyakazi huyo sebuleni inamshushia thamani yake, pia ni rahisi kufanyiwa vitendo vibaya.

“Hivyo naomba waajiri waelewe kwamba anapaswa kuwa na chumba chake tena chenye kitasa kizima kwa kuwa tumeshuhudia wengi vitasa vya milango ya wafanyakazi hawa huwa vinakuwa vibovu wakati wote jambo ambalo sio sawa,” amesema Zanini


Likizo yenye malipo

Likizo yenye malipo ni sehemu ya vipengele hivyo, kikiwataka waajiri kuwalipa wafanyakazi hao wanapokwenda likizo, huu nao ni mtihani mwingine kwa waajiri.

Nasra Selemani amesema ni muhimu jambo hilo lizingatiwe, kwa kuwa mara nyingi mfanyakazi wa majumbani hapewi likizo hadi anaamua kuongopa ili apate mwanya wa kurudi kwao.

“Tunaomba suala la likizo lizingatiwe, kwani hata sisi ni binadamu kuna muda tunahitaji kupumzika, hivyo kama nyie mnavyopewa likizo ofisini kwenu nasi mnapaswa kututendea hayo pia,” anasema Nasra.

Lakini James Urio wa Mbezi Dar es Salaam amesema ni vigumu kumlipa mfanyakazi huyo likizo kwa kuwa anakuwa nje ya sehemu ya majukumu yake ya kazi.

Wakati Urio akieleza hivyo, Mkuu wa Idara ya Sheria wa Chama cha wafanyakazi wa Majumbani Hifadhi, Mahotelini, Huduma za jamii na Ushauri (CHODAWU), Asteria Mathias amesema kama mwajiri anaona kumpa likizo mfanyakazi atapoteza, anapaswa kutafuta mbadala ili mwingine akapumzike.

Ashura Imamu, anasema kumpa mfanyakazi hela ya likizo ni vigumu kutokana na ukweli kwamba hata hao wajiriwa wengi wanaopewa likizo maofisi hawapati haki hiyo.

Mapumziko ya wiki

Kipengele kingine ni mfanyakazi wa nyumbani anatakiwa kupewa siku moja ndani ya wiki kwa ajili ya kupumzika kwa saa 24.

Hiyo siku, mwanasheria wa Chodawu, Wagala Shungu amesema mfanyakazi huyo hapaswi kushika chochote kinachohusiana na kazi hadi saa hizo zitakapokamilika.

Amesema kama kutakuwa na sababu za msingi za kutopumzika, anapaswa kulipwa malipo ya ziada.

Mkazi wa Magomeni, Naomi Joseph amesema itawezekana kama waajiri watapewa elimu ya haki za wafanyakazi hao.

“Elimu tu hapa naona ndio muhimu, kwani bado wafanyakazi hawa watu waliwaweka daraja la chini kiasi cha kuwanyima haki zao na kuonekana ni watu wanaotakiwa kufanya kazi saa zote, tuendelee kupeana elimu bila kuchoka,” amesema Naomi.


Posho saa za ziada

Kwa mujibu wa Chodawu, unapomfanyisha kazi mfanyakazi wako wa nyumbani nje ya saa za kazi zinazojulikana kiserikali unapaswa kumlipa.

Kwa mujibu wa sheria za kazi, saa za kufanya kazi ni tisa. Hata hivyo sheria hii haitekelezwi na waajiri wengi.

Kwa mujibu wa Chodawu, hata pale mfanyakazi huyo anapoamka usiku kumfungulia mume wa bosi wake mlango, anapaswa kumlipa kwa kuwa ni nje ya muda wa kazi.

“Utakuta mama kalala, mume anaporudi msichana wa kazi ndio anaenda kufungua geti au mlango, hii ni sawa na kumfanyisha kazi ya ziada, hivyo unapaswa kumlipa,“ amesema Wagala ambaye ni mwanasheria wa Chodawu.


Mafao

Kama ulidhani mfanyakazi wa ndani hana haki ya mafao, hii inakuhusu. Kisheria wafanyakazi hawa wanapaswa wanapaswa kuwa na mafao, ingawa wengi hulipwa fedha mkononi.

Pia kikwazo kingine katika kuchangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, ni kima chao cha chini cha mshahara wengine huwa kidogo, kisichostahili kukatwa.

Kwa mara ya mwisho kima cha chini kilichotangazwa kwa wafanyakazi hao wa majumbani ni Sh60,000 kwa wale wanaoishi nyumbani kwa mwajiri.

Hivyo akikatwa Sh30,000 ni wazi kwamba atabakiwa na Sh30,000 fedha ambayo hawezi kutosheleza mahitaji yake ya msingi kwa mwezi.