Mambo matano atakayoanza nayo Mwakatobe AICC

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Christina Mwakatobe , akizungumza na waandishi wa habari, aliporipoti rasmi kazini leo Machi 22, 2024. Kulia ni aliyekuwa mkurugenzi wa kituo hicho, Ephraimu Mafuru aliyehamishiwa TTB.

Muktasari:

Christina Mwakatobe aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Machi 18, 2024, akichukua nafasi ya Ephraim Mafuru aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Arusha. Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Christina Mwakatobe,  ametaja mambo matano anayotarajia kuegemea katika uongozi wake ili kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya utalii wa mikutano.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuongeza mapato ya taasisi hiyo, kubuni miradi mikubwa ya maendeleo, lakini pia kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake na kuboresha huduma za taasisi hiyo za mikutano, hospitali na malazi.

Mengine ni kushirikiana na wafanyakazi wenzake wa kituo hicho kuhakikisha pia wanaboresha uhusiano kwa wadau wa utalii nchini.

Mwakatobe aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (Kadco), aliteuliwa aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa AICC, Machi 18, 2024, akichukua nafasi ya Ephraim Mafuru aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Akizungumza leo Machi 22, 2024 jijini Arusha wakati wa makabidhiano ya ofisi hiyo, Mwakatobe amesema anatarajia kuongeza vyanzo vipya vya mapato na kubuni miradi pia kuboresha zilizopo ikiwemo huduma ya mikutano, nyumba za malazi na Hospitali.

“Kujenga uhusiano mzuri baina ya wadau wa utalii na kuboresha huduma zetu,  ni sehemu pia ya malengo yangu bila kusahau maslahi ya wafanyakazi wetu, kwani hayo ndio yatakayoleta uhalisia wa kitovu cha diplomasia ya mikutano na utalii pia” amesema Mwakatobe.

Awali akikabidhi ofisi hiyo, aliyekuwa mkurugenzi wa kituo hicho, Mafuru amesema kuwa anajivunia kuacha ofisi yake ya zamani kwa mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza mapato kutoka Sh11.4 bilioni mwaka 2019/2020 hadi Sh12.78 mwaka 2022/2023 mwezi Aprili.

“Mbali na hilo kuna zaidi ya miradi 16 iliyokuwa imekufa na imeanza kutekelezwa ikiwemo nyumba za makazi, lakini pia ujenzi wa kituo kipya cha mikutano cha Kilimanjaro. Pia upanuzi wa kituo cha Julius Nyerere kilichoko jijini Dar es Salaam,” amesema Mafuru.