Rais Samia amteua bosi mpya AICC kutoka Kadco

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Christine Mwakatobe kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Christine Mwakatobe kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Kabla ya uteuzi huo, Christine alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (Kadco). Ameongoza Kadco kwa mwaka mmoja na miezi sita kuanzia Septemba 1, 2022.

Christine anachukua nafasi ya Ephraim Mafuru ambaye Machi 15, 2024, Rais Samia alimteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Uteuzi wa Christine umetangazwa leo Jumatatu, Machi 18, 2024 na Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.