Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utata Kadco kuendelea na kazi KIA

Muktasari:

  •  Utata huo umeibuka ikiwa imepita miezi sita tangu Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipokabidhi majukumu yake TAA na kuwahakikishia wafanyakazi wa KADCO usalama wa ajira zao

Dar es Salaam. Utata umeibuka katika Kampuni ya Uendeshaji na Uendelezwaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (Kadco), kuendelea kutekeleza majukumu yake wakati Serikali ilishahamisha majukumu yake kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) tangu Novemba 10, 2023.

Utata huo umeibuka ikiwa imepita miezi sita tangu Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipokabidhi majukumu yake TAA na kuwahakikishia wafanyakazi wa Kadco usalama wa ajira zao.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa Kadco imeendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida.

Hatua ya Kadco kutoa taarifa yake Machi 10, 2024 ikitoa siku 21 kwa wananchi 1,712 wa vijiji vinane waliovamia eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuondoka ili kupisha shughuli za uendelezwa wa uwanja huo, ni miongoni mwa mambo yanayozua utata.

Wananchi hao ambao ni wa vijiji vya Sanya station, Tindigani, Chemka, Mtakuja, Majengo kati, Samaria na Malula  wanapaswa kuondoka ndani ya eneo hilo kuanzia Machi 11 hadi Machi 31 ikiwa ni pamoja na kubomoa nyumbani zao, kuondoa mifugo, mazao na usitishwaji wa shughuli zozote za kilimo kwa gharama zao wenyewe.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Christine Mwakatobe imeeleza kuwa, wale wote watakaokaidi maelekezo hayo, wataondolewa ifikapo Aprili mosi, mwaka huu na watalipa gharama zote zitakazoambatana na kazi hiyo.

"Kufuatia kukamilika kwa uthamini wa maendelezo yaliyofanyika juu ya ardhi ya eneo la kiwanja cha ndege na ulipwaji wa kifuta jasho kwa wananchi 1,712, waliokuwa wanaishi ndani ya eneo la KIA ili kupisha shughuli za uendelezaji wa kiwanja kwa masilahi mapana ya Taifa kama alivyoelekezwa na Baraza la Mawaziri Aprili 30, 2022."

Sakata la uwanja wa ndege wa KIA

"Wananchi wote mnaoishi katika vijiji tajwa mnapewa notisi ya siku 21 kuanzia Machi 11 hadi Machi 31 mwaka huu kuondoka katika eneo la kiwanja cha KIA sambamba na ubomoaji wa nyumba, uondoaji wa mifugo, mazao na usitishwaji wa shughuli zote za kilimo kwa gharama zenu kama ilivyoelekezwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha kwa pamoja, mnamo Machi 6 mwaka huu," imesema taarifa hiyo.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20, Kadco na wananchi wa vijiji hivyo wako katika mgogoro wa kugombea ardhi na kwa miaka kadhaa, viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo mawaziri, walifika katika eneo hilo kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Kufuatia hatua hiyo, jana Mwananchi lilimtafuta Waziri wa Uchukuzi, Profesa Mbarawa kuhusu utata huo kumtaka mwandishi kumuuliza katibu mkuu wa wizara hiyo.

“Muulize katibu mkuu atakupa ufafanuzi, yeye ndiye anahusika na hiyo. Siku njema,” alisema na kukata simu.

Alipopigiwa simu juzi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Godius Kahyarara alimtaka mwandishi kufika ofisini kwake Dodoma jana.

Jana alipopigiwa simu, alisema hawezi kuonana na mwandishi kwa kuwa ana vikao vya maandalizi ya bajeti.

“Mimi niko kwenye vikao bado. Kwani mtaka kuandika nini kuhusu Kadco? Tupe nafasi halafu tutaona, kuliko kujadili vitu vinavyofanyiwa kazi.

“Mimi nikushauri, hiyo story yako ui-hold (uizuie) ili utupe nafasi, tukimaliza tutawaita. Sasa hivi tuko kwenye bajeti,” alisema.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Christine Mwakatobe alipoulizwa juzi alisema suala hilo aulizwe Waziri wa Uchukuzi.


Novemba 10, 2023 Profesa Mbarawa aliongoza makabidhiano ya uwanja huo mkoani Kilimanjaro kutoka Kadco kwenda TAA.

Alisema Serikali itazingatia stahiki zote za wafanyakazi zinalipwa kulingana na sheria.

“Kiwanja cha KIA ni kiwanja cha kimkakati pamoja na mabadiliko yaliyofanyika tayari kuna kikosi kazi kinatakachohakikishwa viwango vya uendeshaji vinaendelea kukua na masilahi ya watumishi yanapatikana kulingana na Sheria za utumishi zilizopo,” alisema.

Waziri Mbarawa alisema mabadiliko ya uendeshaji yaliyofanywa yanakwenda sanjari na maboresho katika usafiri wa anga yanayojikita katika ununuzi wa ndege mpya na ujenzi wa viwanja vya ndege ili kurahisisha shughuli za kibiashashara ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso alisema ni wakati sasa wa Serikali kuhakikisha miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege ambayo iko chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na TAA inasimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na viwango.

Makabidhiano hayo yalifanyika baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha azimio lililoitaka Serikali kukabidhi majukumu ya Kadco serikalini.


Ilipotokea Kadco

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Uchukuzi, Kadco ni kampuni iliyosajiliwa Machi 11, 1998 kwa mujibu wa Sheria za Kampuni, Sura ya 212.

Hata hivyo, kutokana na uendeshaji usioridhisha wa uwanja huo, mwaka 2010 Serikali iliamua kununua hisa za wanahisa wenza wa Kadco kwa kuvunja mkataba wanahisa hivyo Kadco kumilikiwa na Serikali asilimia 100.