KADCO yatoa sababu taa za uwanja wa ndege kushindwa kufanya kazi

Hai. Hitilafu  ya umeme iliyojitokeza jana katika taa za kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kusababisha ndege kushindwa kutua  na kuondoka kwa saa kadhaa katika uwanja huo unatajwa kusababishwa na hitilafu ya mradi wa ukarabati mkubwa wa mfumo wa taa za kuongozea ndege ambao unafanywa na kampuni ya CEGI kutoka nchini Hispania.

Akitoa taarifa hiyo leo Oktoba 4, 2023 Mkurugenzi Mkuu wa Menejimenti ya Uendeshaji na uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), Christine Mwakatobe amesema hitilafu hiyo ilidumu kwa saa tatu kisha huduma kurejea.

"Hitilafu hiyo ilidumu takribani saa tatu ambapo hali ya uwakaji wa taa hizo ilirejea kama kawaida, hitilafu hii imetokana na mradi unaooendelea wa ukarabati mkubwa wa mfumo wa taa za kuongozea ndege kiwanjani hapa.

“Mawanda ya mradi huu ni kubadilisha mfumo wote wa zamani wa taa za kuongozea ndege na kuweka mfumo mpya na wa kisasa. Lengo likiwa ni kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa za kuzimika kwa taa katika uwanja huo zilianza kusambaa jana usiku katika mitandao ya kijamii huku iklihusisha ndege ya kampuni ya KLM kushindwa kutua katika kiwanja hiko kutokana na changamoto hiyo.

Hata hivyo, KADCO imesem,a abiria wote waliopata usumbufu kutokana na kadhia hiyo walishafanyiwa utaratibu wa kukamilisha safari zao.

Aidha, katika taarifa hiyo menejimenti ya KADCO inmeomba radhi kwa abiria wote walioathirika kwa namna moja au nyingine kutokana na kadhia hiyo.