VIDEO: Serikali yakubali yaishe, yaing’oa Kadco KIA

Muktasari:

  • Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alitoa tamko hilo jana bungeni, wakati akisoma taarifa yake mbele ya wabunge baada ya mvutano uliochukua mwaka mmoja, huku wabunge wakitaka TAA ichukue jukumu la Kadco ambayo ilikuwa na jukumu la uendeshaji.

Dodoma. Hatimaye Serikali imekubali yaishe kwa kutangaza kuanzia leo itakabidhi shughuli za uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kutoka kwa kampuni ya uendelezaji uwanja huo (Kadco).

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alitoa tamko hilo jana bungeni, wakati akisoma taarifa yake mbele ya wabunge baada ya mvutano uliochukua mwaka mmoja, huku wabunge wakitaka TAA ichukue jukumu la Kadco ambayo ilikuwa na jukumu la uendeshaji.

Mwishoni mwa wiki wabunge waliibua jambo hilo walipokuwa wakichangia hoja za Kamati tatu za Bunge, Uwekezaji wa Mitaji (PIC), Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC) kwenye taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Wabunge walichachamaa kuhusu kampuni hiyo kuendelea kuwa na mamlaka ya kuendesha KIA wakitaka shughuli zikabidhiwe kwa TAA.

Hoja za wabunge zilitokana na Azimio la Bunge la Novemba 4, 2022 walipotaka Kadco iache kujishughulisha na kazi za ndani ya KIA na kwamba ilitakiwa kukabidhi shughuli zote mapema iwezekanavyo, lakini hadi jana ikiwa zimepita siku 373 hakukuwa na makabidhiano yaliyofanyika.

Katika mabishano hayo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi kutolea ufafanuzi nani alikuwa anamiliki KIA kati ya Kadco na TAA na hadi kufikia hatua ya kulumbana.

“AG naomba unisaidie nani alikuwa mmiliki wa KIA kabla ya Kadco ili tupate mahali pa kuanzia, naomba kama ni wewe au Waziri mmoja anipe uelewa huo ili kwa pamoja tujue pa kuanzia,” alisema Spika Tulia.

Sakata la Uwanja wa Ndege KIA latua bungeni

Waziri Mbarawa alimjibu Spika Tulia, kabla ya kupelekwa Kadco, uwanja huo ulikuwa ni mali ya Serikali, lakini wakati wa ubinafsishaji, iliundwa kampuni na baadhi ya watu walijiunga katika sekta binafsi wakaingia katika mkataba.

“Mheshimiwa Spika, nafurahi kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba, kesho (leo) Novemba 10, 2023 Kadco itakabidhi shughuli zake kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege moja kwa moja kama ambavyo Bunge lilielekeza tangu mwaka jana,” alisema Profesa Mbarawa.

Wabunge

Mara baada ya kusomwa kwa kauli ya Waziri, Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafue aliomba mwongozo wa Spika akimtaka awaamuru Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuta kauli zao walizozitoa kabla kwamba jambo la kumuondoa Kadco lilikuwa gumu.

Akijibu mwongozo huo, Spika Tulia alisema hana sababu za kuwahoji au kutaka wasahihishe taarifa zao, badala yake akataka kauli ya Waziri aliyoitoa isimame kuwa ndiyo msimamo wa Bunge kuhusiana na jambo hilo.

Akichangia mpango wa Taifa wa maendeleo 2024/25, Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospiter Muhongo alisema kuna mambo matatu ambayo yanaweza kusaidia kufikia malengo kwa mpango wa 2024/25, akiyataja mambo hayo ni matumizi ya gesi asilia, helium na uvunaji wa hewa ya ukaa, lakini akasisitiza mpango uonyeshe matumizi ya umeme kwa mtu mmoja ni kiasi gani.

Kwa upande wake, Ester Matiko alisema mpango unaweza kufeli na kushindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa kutokana na kushindwa kufikia malengo kwa vitu vingi ambavyo Serikali inalenga kuvifanya, ikiwemo idadi ndogo ya upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa.

Matiko alisema Serikali imesajili Watanzania 24 milioni tangu mpango huo ulipoanza kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi.

Alisema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ilipaswa wawe wamesajili na kutoa vitambulisho kwa Watanzania 35 milioni ambao wana sifa ya kupewa vitambulisho, huku akilalamikia suala la mtambo wa kuchapa vitambulisho kwamba limekuwa ni suala la kudanganya kila wakati.

Kuhusu namna gani Tanzania inaweza kujinasua, alisema ni muhimu ikawekeza hata kwenye uwekaji wa gesi kwenye magari kwa ajili ya kubana matumizi kama inavyoshauriwa.