Mbowe, Profesa Mbarawa wavutana kuhusu Kadco

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Kushoto) na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe (Kulia)

Muktasari:

Pia alihoji kwanini Serikali imetenga hekta 11,000 kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo wakati wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wana shida ya ardhi.

Dodoma. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe amembana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitaka kujua nani mmiliki wa Kampuni ya Uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kadco).

Pia alihoji kwanini Serikali imetenga hekta 11,000 kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo wakati wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wana shida ya ardhi.

Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), alitoa shilingi katika mshahara wa waziri wakati wa upitishwaji wa bajeti ya wizara hiyo kifungu kwa kifungu na aliungwa mkono na Mbunge wa Vunjo (NCCR–Mageuzi), James Mbatia na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT – Wazalendo), Zitto Kabwe wakitaka waziri atoe maelezo ya kwanini uwanja huo umetengewa hekta zote hizo.

“Natoa shilingi kama sitapata majibu ya kueleweka kwa kuwa nimekuwa nikiuliza suala hili la Kadco na hekta hizo kwa miaka 14 tangu nimeingia kwenye Bunge hili,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Waziri (Dk Harrison) Mwakyembe analijua hili, nimelihoji vya kutosha kwa kuwa hata Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow na mingine kama Chicago na dunia nzima hakuna uwanja uliotengewa hekta 11,000 wakati watu wana shida ya ardhi.”

Akijibu hoja hiyo, Profesa Mbarawa alisema Serikali ina mpango wa muda mrefu wa uwanja huo wa Kia, hivyo haiwezi kufanya mabadiliko na uamuzi utabaki kuwa hivyo.

Jibu hilo halikumridhisha mbunge huyo wa Hai ambaye alisimama tena akitaka waziri atoe ahadi ya kufanya mazungumzo kuhusu suala hilo na pia kumtaja mmiliki wa Kadco.

Zitto alimshangaa Mbarawa kusema Serikali ina mpango wa muda mrefu wa eneo hilo wakati wakazi wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, hasa Arumeru, wamekuwa wakilia kuhusu ardhi na wabunge wa maeneo hayo wamekuwa wakihoji mara kwa mara.

Kutokana na hoja hizo, mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu aliingilia kati suala hilo akitaka Waziri Mbarawa kutoa ahadi ya kufanya mazungumzo na Mbowe ili kufikia makubaliano.

Hata hivyo, Profesa Mbarawa alirudia kauli yake ileile ya kuwa na mpango wa muda mrefu wa eneo hilo, majibu ambayo pia yalitolewa na naibu wake, Edwin Ngonyani.

Majibu hayo yalimnyanyua tena Mbowe na kumweleza Zungu kuwa kama mawaziri hawawezi kutoa majibu hayo basi ahoji tu wabunge na mjadala uishe. Zungu aliwahoji na wengi kupinga hoja ya Mbowe.