Mamia wajitokeza kumpokea Rais Samia

Sunday June 13 2021
samia pic
By Saada Amir

Mwanza. Wakazi wa Jiji la Mwanza, viongozi na watendaji wa taasisi na mashirika ya umma  wamejitokeza kwa wingi kumlaki Rais Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuanza ziara ya siku tatu mkoani Mwanza leo Jumapili Juni 13, 2021.

  

Mamia ya watu wamefika katika viwanja vya kiwanda cha kuchenjua dhahabu eneo la Sabasaba na Benki Kuu (BoT) barabara Makongoro ambako Rais Samia anatarajiwa kutembelea katika siku ya kwanza ya ziara yake itakayohitimishwa Juni 15, 2021.

Kiwanda cha kuchenjua dhahabu kimejengwa na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kwa kushirikiana na kampuni ya Rozella ya nchini Dubai kwa gharama ya zaidi ya Sh10.4 bilioni huku jengo la BoT likiwa kimegharimu zaidi ya Sh42 bilioni.

Akiwa mkoani Mwanza, Rais  Samia atatembelea, kukagua na kuzindua mradi wa maji wilayani Misungwi uliotekelezwa kwa zaidi ya Sh13.7 bilioni.


Advertisement

Kiongozi huyo Mkuu wa nchi pia ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kuanzia eneo la Fela wilayani Misungwi hadi Isaka Shinyanga utakaogharimu zaidi ya Sh3.067 trilioni.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, Rais Samia pia atatembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la JPM maarufu daraja la Kigongo-Busisi linalounganisha eneo la Kigongo Wilaya ya Misungwi na Busisi wilayani Sengerema.


Advertisement