Mamia waupokea mwili wa Lowassa Kilimanjaro

Msafara wa magari yaliobeba mwili wa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ukiondoka katika uwanja wa ndege wa KIA kuelekea Monduli. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Safari ya kuelekea katika makazi yake ya kudumu kwa mwili wa Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, hayati Edward Lowassa inaendelea baada ya mwili wake kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Moshi. Mwili wa Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, hayati Edward Lowassa umewasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Baada ya kuwasili, msafara wa kwenda kijijini kwake Ngarash, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha umeanza. Msafara huo una zaidi ya magari 100 likiwemo la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililoubeba mwili huo.
Mwili huo umewasili KIA leo Alhamisi, Februari 15, 2024 saa 5:22 asubuhi ukitokea Dar es Salaam na kupokelewa na waombolezaji mbalimbali wakiwemo wakuu wa mikoa (RC), Nurdin Babu wa Kilimanjaro, John Mongella wa Arusha na Waziri Kindamba wa Tanga wakiwa na kamati zao za usalama.
Ndege ya Serikali ndiyo ilibeba mwili wa Lowassa ikitanguliwa na ndege mbili za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zilizowabeba waombolezaji mbalimbali wakiwemo viongozo wa Serikali, wasanii, ndugu, jamaa na marafiki.
Mwili huo ulishushwa katika ndege saa 5:35 asubuhi na askari wa JWTZ, kisha wakauweka kwenye gari maalumu. Pia, ndege hiyo iliwabeba baadhi ya wanafamilia akiwemo mjane wa Lowassa, Regina na mtoto wake mkubwa, Fredrick pamoja na wajukuu zake.
Baada ya kushuka, mama Regina aliongozana na wakuu hao wa mikoa, Mongella, Kindamba na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro (mwenyeji), Babu kuteta naye huku wakielekea katika magari yaliyoandaliwa.
Baada ya kupanda katika magari, msafara ulianza kuelekea Monduli.
Lowassa (70) alifariki dunia, Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
Taarifa ya msiba huo ilitangazwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango kwa niaba ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Mwili huo wa Lowassa utazikwa Jumamosi ya Februari 17, 2024 na Rais Samia ataongoza waombolezaji katika kuhitimisha safari ya mwisho ya Lowassa hapa dunia.
Baada ya mwili huo, kuwasili kijijini kwake, shughuli mbalimbali zitafanyika leo na kesho Ijumaa zikiwemo za wananchi kuuaga pamoja na kuagwa kimila.
Mapema leo asubuhi, gari la matangazo lilikuwa likipita viunga mbalimbali vya Jiji la Arusha kuwaomba wananchi kujitokeza barabarani pindi mwili huo utakapokuwa ili kupata fursa ya kumuaga mpendwa wao.
Mkazi wa Tukuyu, mkoani Mbeya, Agustino Safe akizungumza na Mwananchi Digital akiwa KIA amesema ameamua kufunga safari kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, kisha Arusha kumzika Lowassa ambaye anamtaja kuwa alikuwa mlezi wake.
“Lowassa alikuwa mtu wa kipekee sana na utaona hivyo kupitia mapokezi anayoyapata," amesema Safe.
Katika moja ya salamu za familia alizozitoa Fredrick, mtoto mkubwa wa Lowassa alisema,“huu msiba si wa kwetu ukoo wa Lowassa, kama wengi walivyokuwa mashuhuda baba amekuwa mlezi, mzazi wa watu wote.
“Tunasema tena na tunarudia watoto na wazazi ambao wanashiriki katika shule za kata leo wanaomboleza, watoto na wazazi ambao wanakunywa maji kutoka Ziwa Victoria leo wanaomboleza, watoto na wazazi ambao leo wanasomesha watoto wao pale UDOM ( Chuo Kikuu cha Dodoma) leo wanaomboleza. Tunasema tunashukuru kwa zawadi ya maisha yake.”
Enzi za uhai wake, Lowassa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo ya Waziri Mkuu wa Tanzania, aliyoihudumu kwa miaka miwili kuanzia Desemba 2005 hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond.
Pamoja na mambo mengine, Lowassa atakumbukwa kwa kuchagiza siasa za upinzani mwaka 2015, alipoamua kujiondoa katika chama alichokulia na kumlea-CCM na kujiunga na Chadema na baadaye kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho, huku akiungwa mkono na vyama washirika vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vikijulikana kwa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Katika uchaguzi huo, ilikuwa mara ya kwanza kwa mgombea wa upinzani kupata kura asilimia 40 ya kura zote na mgombea CCM, John Magufuli alipata kura asilimia 58.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi