Milima, mabonde safari ya Lowassa kuusaka urais tangu mwaka 1995

Muktasari:

  • Ni mwasisi wa kundi la ‘Boys 2 Men’ kati yake na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Uamuzi wa kukatwa jina lake ndani ya CCM 2015 hakufurahishwa nao na kuamua kutimkia Chadema. Moja ya maneno yake jukwaani ni kutoridhishwa na kutoungwa mkono na Kikwete kwenye uchaguzi.

Moshi. Waziri Mkuu aliyejiuzulu wadhifa huo, Edward Ngoyai Lowassa amefariki dunia jana Jumamosi, Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango, wakati akitangaza kifo chake amesema Lowassa (70) amefariki dunia akiendelea na matibabu ya magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.

Hii inamaanisha hatutamuona tena katika ulimwengu huu, lakini Watanzania watakumbuka nguvu ya kisiasa aliyokuwa nayo na safari yake ya kuusaka urais ilivyoanza mwaka 1995.

Uchaguzi siku zote huja na mvumo wake, lakini uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995 na ule wa 2005 ndiyo ulikuwa na mvumo mkubwa kutokana na kuibuka kundi la ‘Boys II Men’ lakini leo mmoja wa wanakundi hatunaye.

Kwa wasiofahamu, kundi la ‘Boys II Men’ liliwahusu marafiki wawili wakubwa wa wakati ule, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa lakini leo Lowassa hatunaye baada ya kufariki dunia akipatiwa matibabu JKCI.

Ni nguvu za wawili hao baada ya kukosa nafasi ya kuteuliwa kugombea urais uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ndipo 2005 wakakubaliana Kikwete ndiye agombee na Lowassa amuunge mkono.

Maandiko mengi ambayo hayajakanushwa kikamilifu, yanasema wawili hao walikubaliana JK aanze mihula miwili (2005-2015), halafu amsapoti Lowassa kuwa Rais kwa muhula unaofuata yaani uchaguzi wa 2015 na ule wa mwaka 2025.

Haikuwa rahisi kupenya mwaka 1995 kutokana na kizingiti cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye tangu walipochukua fomu za urais wakasafiri pamoja kwa ndege, kwani inaelezwa hakuupenda urafiki wa wawili hao.

Lowassa inaelezwa ndiye aliutaka sana urais mwaka ule lakini aliamua kujificha nyuma ya Kikwete kwa sababu Nyerere alikuwa ameshatilia shaka uadilifu wake, kutokana na utajiri aliokuwa nao licha ya kwamba si dhambi kuwa tajiri.

CCM ikarejesha majina matatu tu ambayo yalipelekwa kwenye ngazi ya juu ya mchujo, jina la Lowassa halikuwapo kwani tayari Baba wa Taifa ambaye aliheshimika sana, inaelezwa alikuwa ametilia shaka utajiri wake.

Katika mzunguko wa kwanza wa kura za maoni, Kikwete aliibuka mshindi kwa kupata kura 534, akifuatiwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye alikuja kuwa Rais kwa kupata kura 459 na mzee Cleopa Msuya aliyepata kura 336.

Hata hivyo, upigaji kura ulienda mzunguko wa pili kwa maelezo kuwa Kikwete hakupata kura zaidi ya asilimia 50 kati ya kura 1,331 zilizopigwa na wajumbe wa CCM, hivyo mzunguko wa pili ulifanyika kati ya wawili wa kwanza, Mkapa akapata 686 na Kikwete 639.

Kwa mujibu wa utafiti wa British Academy, matokeo hayo yalikuwa na utata na yalipingwa na kulikuwa na hisia kuwa Nyerere ndiye aliingilia kati na kuhakikisha Mkapa anasimama kugombea urais.

Kulingana na matokeo hayo ilikuwa ni dhahiri kuwa Nyerere hakuwa anajua vizuri nguvu ya ‘Boys II Men’ kwa sababu kama angeijua, asingeruhusu Kikwete afike mbali kiasi hicho kwenye kura na wawili hao hawakuacha matamanio yao ya urais.


Kupanda, kushuka kwa wanamtandao

Nyerere anachukuliwa kama mwadilifu na aliyetumika kuvunja makundi yasiyo rasmi kuchukua madaraka mwaka 1995. Alifariki dunia Oktoba 14, 1999 hapo ndipo zilipozaliwa siasa mpya ndani ya CCM kwa kuzaliwa mitandao minne.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofadhiliwa na British Academy na DFID za Uingereza, kifo cha Nyerere kilishuhudiwa ikizaliwa mitandao minne ikitafuta urais 2005 baada ya Mkapa na mmoja ni kundi la Boys II Men la Lowassa na Kikwete.

Inaelezwa katika utafiti huo kuwa kundi hili liliendelea kujipenyeza ndani ya mifumo ya CCM, lilifanikiwa kuwaingiza katika mtandao huo, Dk Emmanuel Nchimbi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Sophia Simba wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT).

Mtandao wa pili ulikuwa ni wa Profesa Mark Mwandosya uliotaka urais uwe zamu ya kusini, kundi la tatu la Waziri Mkuu, Frederick Sumaye na kundi la nne lilikuwa la Waziri Mkuu mstaafu na mwenyekiti mstaafu wa OAU, Salim Ahmed Salim.

Uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ulipowadia, Lowassa na Kikwete kila mmoja akawa anautamani urais, kiasi kwamba kama si mzee Peter Kisumo kuingilia kati na kukutana nao,  kuwataka wakubaliane kuachiana, pengine wangegawana kura.

Kundi hili la ‘Boys II Men’ na mtandao wake likafanya kazi kubwa hadi Kikwete akaibuka kidedea kwa kupata kura za kishindo katika mchujo ndani ya CCM mwaka 2005 zikiwa 1,072, Salim kura 476 na Profesa Mwandosya akapata kura 122.


Boys II Men likatoa spika, waziri mkuu

Mbali ya Kikwete na Lowassa, lakini mtandao huo uliwajumuisha vigogo kama, Rostam Aziz na Nazir Karamagi waliokuwa wafanyabiashara mashuhuri, Samwel Sitta, Dk John Nchimbi, Sophia Simba na Kisumo waliokuwa na nguvu kubwa kisiasa.

Kundi hilo ndilo inaelezwa lililopanga Sitta awe Spika wa Bunge la tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Lowassa awe Waziri Mkuu na hata wakati Sitta anasoma bungeni jina la waziri mkuu ili lipigiwe kura, halikuwa geni.

Ni katika kipindi cha utawala wa Kikwete ndipo kundi la wanamtandao lilipoanza kuparanganyika na kukiletea CCM wakati mgumu katika uchaguzi mkuu wa 2010 na ule wa 2015, Lowassa na Kikwete wakaanza kuhitilafiana.

Bunge chini ya Sitta likamsulubu Lowassa kutokana na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe, kuhusu kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, hadi Lowassa akaamua kujiuzulu uwaziri mkuu, Februari 7, 2008.


Lowassa na uchaguzi mkuu 2015

Hadi kuelekea uchaguzi mkuu 2015, inaelezwa ndani ya CCM, Kikwete alikuwa amesimama upande wa Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati ule, Bernard Membe, huku Lowassa akibebwa na mitandao mingine ukiwemo Friends of Lowassa.

Wanamtandao wawili waliobebana 1995 na 2005 ndio sasa walikuwa wakichuana na kupingana na mwisho wa siku, Lowassa ndiye aliyepoteza vita hiyo.

Lowassa jina lake lilikatwa mapema hata hakufika kwenye tano bora, lakini kwa vile aliutaka urais kufa au kupona, alijiunga na Chadema na kuteuliwa kupeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini akaangushwa na hayati Dk John Magufuli.

Katika kampeni zake, Lowassa hakuacha kuficha hisia zake pale aliposema majukwaani kuwa alitarajia Kikwete angemuunga mkono ndani ya chama 2015, lakini alimgeuka, na ni mvurugano wao ndiyo uliomuibua Dk Magufuli na kuwa Rais.

Lowassa alinukuliwa akisema alitarajia Kikwete angemsaidia kwa vile walikuwa na makubaliano kwamba yeye amsaidie 2005 ili aweze kushinda na ndiyo maana wala hakumpinga 2010, akiamini uchaguzi wa 2015 naye angemuunga mkono. Baada ya kuangushwa na Dk Magufuli na Ukawa iliyokuwa na vyama vinne CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na Chadema kugomea kutambua matokeo hayo na kukawa na vuguvugu la kuitisha maandamano makubwa nchini, ni Lowassa ndiye aliyetuliza joto hilo aliponukuliwa akisema hautaki urais wa damu.

Akiwajibu wale waliotaka yeye, Chadema na Ukawa waingie barabarani, Lowassa alisema kama angefanya hivyo, wangekuwa wanakwenda Ikulu kwa kumwaga damu za Watanzania wasio na hatia ambao wangepata madhara.

“Tutakuwa tunakwenda Ikulu kwa kufagia barabarani kwa damu za watu. No (hapana), Tutakwenda Ikulu bila damu za watu wakati wowote na Mungu atatusaidia. Nawaambia wale wote ambao hawakuridhika, mnajua nguvu ya umma lakini msiitumie kuwaumiza watu,” alinukuliwa Lowassa akisema.

Baadaye Machi 1, 2019, Lowassa akatangaza kurejea tena CCM na hadi anafariki dunia alikuwa mwanachama safi wa chama hicho tawala. Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina Lake Lihimidiwe. Pumzika kwa amani Lowassa.