Manusura waeleza magumu waliyopitia

Muktasari:

Waeleza jinsi walivyookolewa kutoka kwenye ndege

Bukoba/Dar. Manusura wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyotumbukia Ziwa Victoria wameelezea jinsi waliyookolewa kwenye ajali hiyo.

Walisimulia tukio hilo wakiwa wamelazwa wodi namba 10 katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera, iliyopo Bukoba.

Akizungumza jana, Richard Komba (41) aliyekuwa abiria kutoka Dar es Salaam alisema wakati ndege ikiwa angani walipofika Mwanza hali ya hewa ilibadilika, kwani wingu lilikuwa limetanda angani.

“Wakati tunakaribia kushuka ikaonekana hatuwezi kushuka wakati huo kwa hiyo rubani akalazimika kuzunguka tunaenda mpaka maeneo ya Misenyi na akatoa taarifa kuwa hali sio nzuri mvua inanyesha, kuna mawingu na tulikuwa tunaona.

“Basi tukawa tunarudi kwa ajili ya kutua, tukatangaziwa baada muda mfupi tutakuwa tumetua, lakini hali ya hewa bado si nzuri, tulikuwa tunashuka lakini mtikisiko ulikuwa mkubwa, lakini baadaye nikajikuta tuko kwenye maji,” alisema na kuongeza:

“Mimi nilikuwa siti ya nyuma mwisho, na wenzangu tuliokuwa nyuma tukawa na sisi tunahangaika, tulikuwa na mhudumu wa ndege naye alikuwa anahangaika kufungua mlango, sasa sijafanikiwa kujua kama alifanikiwa au nani, basi tukajikuta tumeanza kutoka.

“Kwa hiyo tulitoka pale nje, lakini hakukuwa na msaada wa haraka kama kuna boti au chombo cha karibu cha kuweza kutuokoa. Ilichukua muda kidogo,” alisema.

Alieleza kuwa baadaye ilikuja boti inayotumia makasia na hata walippoanza kuingia walipata wasiwasi wa kuzama kutokana na wingi wa watu, lakini baadaye boti nyingine zilifika na kufanikiwa kutoka.

Kwa upande wake, Theodora Mpesha (46) ambaye amejeruhiwa sehemu ya jicho alisema ni Mungu ndiye amemuokoa, kwani ilipotokea ajali kwenye ndege giza lilikuwa limetanda na maji yalijaa na yeye alikuwa amefunga mkanda.

Alisema baadaye aliwaona wenzake wakikimbia kuelekea mlangoni, ndipo naye akili alimjia akafungua mkanda na kwenda upande ulipokuwa mlango na kufanikiwa kuingia kwenye mtumbwi hadi hospitali.

“Wakati nikiwa kwenye ndege giza lilitanda ndani na maji yakajaa, hivyo tukawa tunaelea, mimi nikiwa bado nimefunga mkanda, akili ilinijia nifungue mkanda nikaelekea wenzangu walipokuwa kwenye mlango, nikabahatika kutoka nje na kuingia kwenye boti na baadaye tukaletwa hapa hospitali ila bado sijisikii vizuri,” alisema Stanslaus.

Salvatory Temba aliyekuwa abiria katika ndege hiyo alisema walipofika kanda ya ziwa walitahadharishwa na rubani juu ya hali ya hewa kuwa mbaya na kadiri walivyoendelea na safari ndivyo ilivyozidi kuendelea kuwa mbaya hatimaye wakajikuta ndege yao imepata ajali.

“Tulitahadharishwa kwenye ndege, ingawa tulijua hali itakuwa shwari, hivyo hatukuvaa jaketi (life jacket) na ajali ilipotokea ndani ya ndege pakajaa maji, abiria tulianza kuhangaika, kila mtu alikuwa anatafuta njia ya kujiokoa,” alisema.

Mmoja wa majeruhi ambaye alikuwa akiokoa abiria, Majaliwa Jackson (20), mkazi wa Nyamkazi manispaa ya Bukoba alisema akiwa katika biashara zake za kuuza dagaa karibu na eneo la ajali aliona ndege ikikuja na baadaye ikarudi hadi kisiwa cha Musira ikapinda kona kwenda Kastam na baadaye ilivyorudi ndipo ikatumbukia kwenye maji.

Alisema sehemu hiyo walikuwepo wavuvi watatu, walishuka na mtumbwi wa kasia wakitokea ziwani na aliona watu wakiamsha mikono kupitia dirishani kama ishara ya kuomba msaada ndipo aliwaomba wenzake waende kuokoa watu.

Jackson alisema alipiga mlango wa ndege ukafunguka na abiria walianza kutokaa na kuingia kwenye mtumbwi wao na wakati akielekea kwenye madirisha mengine kuona kama anaweza kupiga kioo alishindwa na hapo alisikia mtu akipiga kioo upande wa rubani akimpa ishara ya kufungua mlango wa dharura.

“Niliokota mkanda kama wa mkoba kwenye maji, ili nifunge kwenye mlango wa dharura wakati nimefunga nikiendelea kuvuta mkanda ulikatika na kunigonga kichwa na mimi nilipoteza fahamu na kudondoka kwenye maji na nilijikuta nimelazwa hospitali ya mkoa. Kwa sasa naendelea vizuri na nimeruhusiwa kutoka hospitali,” alisema Jackson.

…amwaga chozi

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mkurugenzi mkuu wa shirika la Precision Air, Patrick Mwanri alijikuta akitoka machozi wakati akielezea ajali hiyo.

Wakati wote alipokuwa akizungumza uso wake ulionekana kujawa na simanzi na alipomaliza kuzungumza alishindwa kuzuia machozi.

Alitoa kitambaa na kufuta machozi mbele ya waandishi wa habari, kisha akanyanyuka na kuahidi atatoa taarifa kadiri watakavyozipata kutoka kwa mamlaka husika.

Katika taarifa yake hiyo alisema jitihada za kuwaokoa watu wote walikuwa kwenye ndege hiyo zinaendelea akieleza lengo ni kuhakikisha wote wanapatikana.

Kulingana na mkurugenzi huyo, ndege hiyo iliyopata ajali ina uwezo wa kubeba watu 48 na waliokuwa ndani ya ndege wakati ajali inatokea ni abiria 39 akiwemo mtoto mchanga na wafanyakazi wanne wa Precision.

MDH yapoteza watumishi watano

Katika ajali hiyo, Shirika la Usimamizi na Maendeleo ya Afya (MDH) limepoteza watumishi watano kati ya wanane waliokuwa wamesafiri na ndege hiyo kwenda Bukoba.

Akizungumza na gazeti hili, mkurugenzi mtendaji wa MDH, Dk David Sando alisema watumishi wanane wa ofisi hiyo walikuwa safarini kwenda Bukoba.

“Watumishi wetu jumla walikuwa wanane na awali walitolewa watatu ambao hali zao hazikuwa nzuri wakapelekwa hospitali, lakini baadaye walitolewa watano ambao hawakuweza kuishi, wamefariki,” alielezea Dk Sando kwa masikitiko.

Alitaja majina ya watumishi waliopoteza maisha ni watafiti watatu wakiwemo Dk Boniface Jullu, Dk Neema Faraja na Dk Alice Simwinga pamoja na Sauli Happymark pamoja na mkuu wa kitengo cha mawasiliano MDH, Zarcharia Mlacha.

Aliwataja watumishi watatu waliofanikiwa kuokolewa ni Nickson Jackson, Dk Josephine Mwakisambwe na Dk Felix Otieno.

Dk Sando alisema wataalamu hao wa afya ya jamii walikuwa wakielekea Tabora wakipitia Mwanza na kwamba lengo la safari hiyo ilikuwa ni mkutano wa mwaka kwenda kuangalia maendeleo ya miradi.

Imeandikwa na Alodia Dominick (Bukoba), Harieth Makwetta na Baraka Loshilaa (Dar)