Maofisa habari waagizwa kuwapa wananchi taarifa za miradi

Msemaji Mkuu wa Serikali, Greyson Msigwa akizungumza wakati maofisa habari, mawasiliano na uhusiano wa Serikalini walipotembelea Bandari ya Tanga.

Muktasari:

Maofisa habari mawasiliano na uhusiano serikalini watembekea Bandari ya Tanga kuona ujenzi wa upanuzi Gati la Bandari hiyo

Tanga. Maofisa habari, mawasiliano na uhusiano serikalini wametakiwa kuitangaza miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali nchini ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi za utekekezaji wa miradi hiyo inayotokana na kodi zao.

Agizo hilo limetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Greyson Msigwa wakati maofisa hao walipotembelea Bandari ya Tanga na kuona maendeleo ya upanuzi Gati la bandari hiyo pamoja na uongezaji wa kina cha bandari.

Amesema Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya bandari ambapo ameitaja maeneo inakotekelezwa miradi hiyo kuwa ni Tanga, Mtwara na Dar es Salaam.

Awali, akisoma taarifa ya maendeleo ya utekekezaji mradi wa upanuzi wa Gati la Bandari ya Tanga, Mhandisi Hamisi Kipalo amesema mpaka umefikia asilimia 45

" Mradi huu unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo kwa awamu ya kwanza ilikuwa ni kuongeza kina, na tumefikia asilimia 98 na hii ni awamu ya pili  ni upanuzi wa Gati," amebainisha  Mhandizi Hamisi.

Aidha utekekezaji wa awamu ya kwanza wa uongezaji wa kina zaidi ya shilingi bilioni 172 zilitumika na awamu ya pili ni bilioni 256.8 na kwamba unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti.

Kwa upande wake Ofisa Habari Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Raya Suleimani amesema amepokea maelekezo ya Msemaji Mkuu wa Serikali na kwamba watayanyia kazi.

"Ni wajibu wetu kutangaza miradi na kazi zinazofanywa na serikali ili wananchi waweze kuwa na taarifa za namna Serikali yao inavyotekeleza miradi mikubwa," amesema Raya.