Maofisa kilimo, wenyeviti wa vijiji wanolewa kukabili nzige wa jangwani
Ofisa Ushawishi na Sera kutoka shirika la Kilimohai Tanzania, Paul Chilewa akizungumza na maofisa kilimo, viongozi wa dini pamoja na wenyeviti wa vijiji Wilayani Mwanga juu ya utambuzi na udhibiti wa nzige wa jangwani. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Maofisa kilimo, viongozi wa dini, wenyeviti wa vijiji wa Mikoa mitatu ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara wametakiwa kuwatambua aina ya nzige ambao ni waharibifu kwenye maeneo yao na namna ya kuwadhibiti endapo watarejea tena nchini.
Mwanga. Maofisa kilimo, viongozi wa dini, wenyeviti wa vijiji wa Mikoa mitatu ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara wametakiwa kuwatambua aina ya nzige ambao ni waharibifu kwenye maeneo yao na namna ya kuwadhibiti endapo watarejea tena nchini.
Februari 19 mwaka jana, Serikali ilitangaza uwepo wa kundi la wadudu aina ya nzige zaidi ya Sh50 milioni walioingia nchini kupitia Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro na baadaye kuelekea Wilaya za Moshi, Siha, Simanjiro, Monduli na baadaye Wilaya ya Longido.
Akizungumza wakati akitoa mafunzo katika Wilaya ya Mwanga juu ya utambuzi na udhibiti wa nzige wa jangwani kwa viongozi hao, Ofisa ushawishi na utetezi sera ,kutoka Taasisi ya kuendeleza kilimohai Tanzania (Toam), Paul Chilewa amesema mafunzo hayo ni muhimu kutokana na kwamba wakati nzige walipoingia nchini mwaka jana wakulima walikuwa hawana uelewa juu ya utambuzi wa nzige hao.
"Tunatoa mafunzo haya na kufanya jitihada za kupunguza madhara endapo nzige wa jangwani watajitokeza tena kwa mara ya pili kama ilivytokea mwaka 2021, kwa hiyo tunawapa elimu na kuwajengea uwezo wataalam hawa wakiwemo Maofisa kilimo wa Wilaya,viongozi wa dini pamoja na wakulima,"amesema na kuongeza
"Elimu hii itawasaidia kujiandaa kwa namna yoyote ile ya kukabiliana na nzige hasa wakulima na tunaamini jamii itajipanga vizuri kutokana na elimu hii tuliyotoa leo kwa viongozi wetu hasa wenye maeneo ambayo mwaka jana nzige hawa waliingia,"amesema Chilewa
"Wilaya zote ambazo zilipitiwa na nzige mwaka jana tutatoa elimu ya namna ya kukabiliana na nzige wa jangwani endapo watajitokeza tena lakini tumehakikisha maeneo yote ambayo yalipitiwa na nzige tunatoa elimu ya kutosha,"amesema
Kwa upande wake Ofisa kilimo wa Wilaya ya Mwanga, Aggrey Maole amesema nzige wengi walienea kwenye Wilaya hiyo kutokana na kwamba wananchi wengi walikuwa hawana uelewa wowote wa namna ya kutoa taarifa na kwamba wangeweza kuwadhibiti mapema kipindi walipoingia nchini.
"Mwaka jana tulipata uvamizi wa nzige kwenye Wilaya yetu na tulikuwa hatuna uelewa kabisa wa namna ya kukabiliana na nzige kwasababu ilikuwa ni mara ya kwanza kwasababu wataalamu wanasema nzige hao walitokea miaka 70 iliyopita,"amesema Maole
"Kwa hiyo mafunzo haya yametusaidia namna ya kutambua aina ya nzige ambao ni wavamizi, uelewa huu tutautumia kuwaelimisha wakulima wa chini kabisa namna ya kutambua nzige endapo wakija kwa mara nyingine tena na itasaidia kutoa taarifa kwa wataalam pamoja kuondoa taharuki kwenye maeneo yetu,"
Juma Mwinyimkuu, Kutoka Wizara ya Kilimo kitengo cha afya ya mimea kanda ya Kaskazini,amesema elimu hiyo ambayo imetolewa itawasaidia wakulima kujiandaa kukabiliana na nzige endapo nzige watatokea kwa mara nyingine.
"Japo hatutegemei kupata nzige siku za hivi karibuni tumeona tuwajengee uwezo wakulima wetu ili waweze kumtambua nzige ili ikitokea nzige hao wakitokea wawe na uwezo wa kumtambua na kuwasiliasha taarifa mahali panapostahili,"amesema Mwinyimkuu
Amesema awali walifanya tathmini kwa wakulima ambapo walibaini wananchi wengi hasa wakulima kutokuwa na uelewa wa nzige hao.