Vigogo wa CWT waendelea kusota rumande, upelelezi haujakamilika
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba.
Muktasari:
- Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wanaokabiliwa na mashitaka ya rushwa na uhujumu uchumi wameendelea kubaki rumande.
Dodoma. Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wanaokabiliwa na mashitaka ya rushwa na uhujumu uchumi wameendelea kubaki rumande baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa bado haujakamilisha upelelezi wa shauri linalowakabili.
Mbali na kutokamilika kwa upelelezi, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwa, bado unasubiri uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ili kubaini iwapo kesi hiyo itasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi au kuhamishiwa Mahakama ya Uhujumu Uchumi.
Shauri hilo limetajwa leo Ijumaa, Juni 19, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Denis Mpelembwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Leah Ulaya, Suleiman Ikomba, Maganga Japhet, Nashon Kidudu, Joseph Misalaba, Baraka Mbonalibha, Wambura Kihengu, Angelina Wambura na Kampuni ya Pyrite and Industries Limited.
Akiwasilisha taarifa ya shauri hilo, Wakili wa Serikali, Jerry Kayumbo, amesema upelelezi bado unaendelea na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na mawakili wa utetezi waliodai kuwa upande wa Jamhuri umeshindwa kutekeleza maagizo ya mahakama yaliyotolewa Juni 8, 2026.
Mawakili hao walidai kuwa mahakama iliutaka upande wa mashtaka kufika leo ukiwa na majibu ya lini upelelezi utakamilika pamoja na hatua iliyofikiwa kuhusu kibali cha DPP, lakini hakuna taarifa mahsusi iliyowasilishwa.
Wakili Meshack Ngamando, amesema kitendo cha upande wa Jamhuri kushindwa kutoa majibu ya maagizo ya mahakama kinaonyesha kutokuwa na uzito katika utekelezaji wa maelekezo ya mahakama.
"Leo tulitarajia kupata majibu ya lini upelelezi utakamilika na kibali cha DPP kitapatikana lini, lakini badala yake tunaombwa tarehe nyingine bila maelezo ya kutosha kuhusu hatima ya wateja wetu," amesema Ngamando.
Amedai kuwa ikiwa upande wa Jamhuri haujawa tayari kuendelea na kesi hiyo, basi washtakiwa wanapaswa kuachiwa huru na kurejeshwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.
"Hawa ni watu wanaofahamika na wana anuani zinazotambulika. Hawatatoroka. Waachieni kwanza, mkikamilisha upelelezi mtawarejesha mahakamani," amesema.
Naye, Wakili Sedrick Mbunda, amesema ni wajibu wa pande zote katika shauri kuheshimu maagizo ya mahakama kwa kuwa ndiyo mhimili unaosimamia utoaji wa haki.
Akitoa maelekezo, Hakimu Mpelembwa ameukumbusha upande wa Jamhuri wajibu wake wa kutekeleza maagizo ya mahakama na kuwasilisha taarifa kamili kuhusu maendeleo ya upelelezi pamoja na kibali cha DPP.
"Mjitahidi kutii amri za mahakama. Mtakapokuja tarehe ijayo, mje na majibu kuhusu kukamilika kwa upelelezi na kibali cha DPP ili shauri liendelee katika mahakama yenye mamlaka ya kulisikiliza," amesema.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Julai 1, 2026 litakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa.