Maofisa Uhamiaji mbaroni tuhuma ya mauaji kijana Kakonko

Kijana Enos Elias (20) enzi za uhai wake. Picha kwa hisani ya familia
Muktasari:
- Kifo cha Enos ambaye enzi za uhai wake alikuwa akijishughulisha na kilimo na ujasiriamali kimegubikwa na utata baada ya kutoweka kwa siku kadhaa kabla ya mwili wake kukutwa ukiwa umezikwa na watu wasiofahamika katika pori la Kichacha Kijiji cha Chilambo kilometa kadhaa kutoka mjini Kakonko.
Kakonko. Maofisa Uhamiaji wanne wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusu kifo chenye utata cha kijana Enos Elias (20), mkazi wa Kijiji cha Ilabilo Wilaya ya Kakonko aliyekuwa akishikiliwa kwa mahojiano kuhusu uraia wake.
Kifo cha Enos ambaye enzi za uhai wake alikuwa akijishughulisha na kilimo na ujasiriamali kimegubikwa na utata baada ya kutoweka kwa siku kadhaa kabla ya mwili wake kukutwa ukiwa umezikwa na watu wasiofahamika katika pori la Kichacha Kijiji cha Chilambo kilometa kadhaa kutoka mjini Kakonko.
Kabla ya kutoweka na baadaye mwili wake kupatikana, kijana huyo aliwapigia simu ndugu zake kuwajulisha kuwa anashikiliwa na maofisa wa Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Kakonko baada ya kutiliwa mashaka uraia wake na kuomba atumiwe namba ya Kitambulisho cha Taifa (Nida) ya mama yake mzazi, Juliet Joseph ili aweze kuthibitisha uraia wake.
Taarifa zilizopatikana kutoka Kakonko na kuthibitishwa na Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Novat Dawson zinasema maofisa wanne wa Uhamiaji Wilaya ya Kakonko wanashikiliwa kwa mahojiani kuhusu kifo hicho.
‘’Ni kweli wanashikiliwa tangu jana (Novemba 17, 2023)…lakini kwa maelezo zaidi kuhusu hilo wasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma ndiye mwenye maelezo ya kutosha,’’ amesema Ofisa Uhamiaji huyo wa mkoa
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Phillemon Makungu kuzungumzia sula hilo hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Maelezo ya familia
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Kijiji cha Ilabilo Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Juliet Joseph, mama mzazi wa kijana Enos amesema yeye, familia na jamii wanaamini kijana huyo amefikwa na mauti akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa vyombo na taasisi za Serikali.
Mama huyo anasema mara ya mwisho kuwasiliana na familia, Enos alikuwa mikononi mwa maofisa Uhamiaji na kuomba uchunguzi kuanzia kwa maofisa waliomkamata na kituo cha polisi Kakonko alikolala kabla ya kukabidhiwa tena kwa maofisa Uhamiaji.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Angel Elias ambaye ni dada wa Enos akisema ndiye aliyezungumza naye kwa njia ya simu Jumamosi Oktoba 28, 2023 akimtaka kumtumia namba ya kitambulisho cha mama yao ili awathibitishe uraia wake kwa maofisa Uhamiaji waliokuwa wanamshikilia.
‘’Wakati nazungumza naye, mimi na mama tulikuwa shambani; na kwa sababu namba ile ilikuwa imeandikwa kwenye karatasi ambayo ilikuwa nyumbani kwa wakati huo, ilibidi mama arejee nyumbani kuichukua lakini tulishindwa kumtumia baada ya simu yake kutopatikana hewani,’’ amesema Angel
Maiti kufukuliwa porini
Akisimulia jinsi mwili wa ndugu yake ulivyopatikana, Angel anasema baada ya kumtafuta kwenye ofisi ya Uhamiaji na Kituo cha Polisi Kakonko bila mafanikio tangu Oktoba 27, 2023 alipokamatwa, Novemba 3, 2023, familia ilipigiwa simu ikitakiwa kufika Kituo cha Polisi Kakonko na kujulishwa kuwa kuna kaburi imeonekana katika pori la Kichacha, umbali wa zaidi ya kilometa 25 kutoka Kakonko mjini.
‘’Tuliongozana na askari hadi porini na baada ya kaburi kufukuliwa na mwili kutolewa, mama aliutambua kuwa ni wa marehemu kaka Enos kutokana na alama iliyokuwa nayo kwenye meno,’’ amesema.
Anasema hadi sasa, familia inajiuliza ni kwanini maofisa Uhamiaji waliomkamata na wenzao wa Jeshi la Polisi alikohifadhiwa baada ya kukamatwa walikana kumshikilia wala kujua taarifa za Enos ambaye tayari amezikwa kwenye makaburi ya umma kijijini hapo Novemba 14, 2023.
Zitto ajitwisha zigo
Kutokana na utata huo, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazaledno, Zitto Kabwe anaefanya ziara ya kichama mkoani Kigoma ametembelea familia ya Enos katika Kijiji cha Ilabila na kuahidi kuwa yeye binafsi na chama chake watashirikiana bega kwa bega na familia kufuatilia hadi sababu, mazingira na wahusika wa kifo cha kijana huyo.
‘’Katika hili sisi ACT-Wazalendo kama taasisi tunalitaka Jeshi la Polisi litimize wajibu kwa kuchunguza kwa kina kifo hiki na wahusika wote kufikishwa mahakamani,’’ Zitto amesisitiza