Maofisa wanne Polisi wadaiwa kuomba rushwa Sh200 milioni

Thursday May 19 2022
pesa pic
By Pamela Chilongola

Dar es Salaam. Shahidi James Wawenje katika kesi inayowakabili maofisa wanne wa upelelezi wa Kituo cha Polisi Kawe, amedai alipokea barua kutoka ofisi ya Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikimtaka atoe taarifa ya namba ya simu ya Diana Naivasha anayedaiwa kuombwa rushwa kwa maofisa hao.
Katika kesi hiyo, Shabani Shillah, Joyce Kitta, Ulimwengu Rashid na Emmanuel Ngeleja wanakabiliwa na mashtaka tisa likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kupokea rushwa zaidi ya Sh15 milioni.
Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Desemba 17, 2018 eneo la Social Club Rainbow Kinondoni washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa maofisa wa upelelezi walishawishi rushwa ya Sh200 milioni kutoka kwa Diana Naivasha wakidai amekamatwa na nyara za Serikali.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Mei 19, Wawenje ambaye ni Meneja wa Ulinzi na Usalama wa kampuni ya simu ya Vodacom, amedai Takukuru walimtaka atoe taarifa ya namba ya simu 0763777999 inayomilikiwa na Naivasha.
Huku akiongozwa na Wakili wa Takukuru, Imani Nitume, Wawenje amedai amedai kuwa alipata barua hiyo Aprili 26, 2019 akiwa katika ofisi ya Vodacom makao makuu iliyopo maeneo ya Morocco.
Amedai baada ya kupokea barua hiyo aliingia kwenye mifumo ya simu ya kampuni hiyo na kuanza kukagua ili kuhakikisha kama ina usalama na kumruhusu kutoa taarifa kama hati inavyoelekeza.
“Niliandaa barua na kumjibu kamanda wa Takukuru na taarifa nilizotoa nilizigonga muhuri wenye jina langu, cheo changu na nilisaini hii barua na nilipomaliza niliikabidhi kwa ofisa wa Takukuru,” amedai Wawenje.
Wawenje amedai baada ya kumkabidhi barua hiyo ofisa wa Takukuru ndipo na yeye alimkabidhi hati ya uchukuaji wavielelezo pamoja na kuandika maelezo ya Takukuru.
Ameendelea kueleza kuwa namba iliyotakiwa kutolewa katika mifumo yao ni 0763777999 ambayo ilikuwa inamilikiwa na Diana Naivasha aliwasiliana na 0657888777 ambayo inamilikiwa na Shaban Shillah kuanzia Desemba 14, 2018, Februari 23, 2019 na Aprili 11, 13, 14, 2019 akiwa kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya Claus Kawe, Cocacola mikocheni, Kinondoni na Bamaga.
Baada ya kutoa ushahidi huo vielelezo vilipokelewa na mahakama hiyo ambapo shauri hilo limeahirishwa hadi leo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Advertisement