Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maombi ya utetezi kesi ndogo ya kina Zumaridi yatupwa

Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi

Muktasari:

  • Maombi yaliibuliwa na jopo la mawakili wa utetezi Septemba 14 mwaka huu, baada ya kuibuka mvutano kuhusiana na saini iliyowekwa kwenye maelezo ya onyo ya mshtakiwa namba moja (Mfalme Zumaridi) aliyedai saini iliyowekwa kwenye maelezo hayo siyo yake.

Mwanza. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza imetupilia mbali maombi mawili yaliyowasilishwa na jopo la mawakili wa utetezi katika kesi ndogo iliyoibuka ndani ya kesi kubwa inayowakabili Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi na wenzake 83.

Maombi hayo yaliibuliwa na jopo la mawakili wa utetezi Septemba 14 mwaka huu, baada ya kuibuka mvutano kuhusiana na saini iliyowekwa kwenye maelezo ya onyo ya mshtakiwa namba moja (Mfalme Zumaridi) aliyedai saini iliyowekwa kwenye maelezo hayo siyo yake.

Akitaja maombi hayo leo Septemba 20, Wakili wa utetezi, Steven Kitale ameieleza mahakama kuwa hawako tayari kuendelea na kesi hiyo kwani hawajakabidhiwa vielelezo ambavyo wameviomba kwa mahakama na Jeshi la Polisi ili kukamilisha ushahidi wao.

Vielelezo vilivyoombwa ni Maelezo ya onyo ya mshtakiwa namba moja (Mfalme Zumaridi) yaliyopokelewa katika kesi ya Jinai namba 10/2022 inayosikilizwa kwa Hakimu Mkazi, Monica Ndyekobora.

Vielelezo vingine ni Kitambulisho cha Taifa (Nida), Mpiga Kura na Hati ya kusafiria ya mteja wake ambavyo vyote vinashilikiwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa.

"Mheshimiwa tulishaandika barua kwa Hakimu Mkazi, Ndyekobora kuomba maelezo ya onyo ya mteja wetu yaliyopokelewa kwenye kesi anayoisikiliza tukaahidiwa kukabidhiwa nakala leo ili tufanye ulinganifu wa saini lakini hadi muda huu hatujakabidhiwa nakala hiyo," ameeleza Kitale

Ameongeza; "Pamoja na maelezo hayo, pia tuliandika barua kwa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, hii hapa (akaionyesha nakala) kuwaomba walete vitambulisho vya mteja wetu kwa ajili ya kutumika kulinganisha saini lakini hatujajibiwa hadi leo,"

Maelezo hayo yalipingwa na Wakili wa serikali mwandamizi, Dorcas Akyoo ambaye ameieleza mahakama kuwa mashahidi wa utetezi wanaweza kuendelea kutoa ushahidi wao bila kuwa na vielelezo hivyo.

Akyoo ameeleza mahakama kuwa awali wakili mwingine wa utetezi, Erick Mutta aliieleza mahakama kuwa upande wa utetezi uko tayari kutoa ushahidi wake huku akisema wana mashahidi watatu katika kesi hiyo.

"Wakili mwenzake (Mutta) hakuieleza mahakama hii mapema kuwa hawatoweza kutoa ushahidi wao kwa kukosa hivyo vielelezo. Hivyo upande wetu tunaomba ombi lao likataliwe kwa sababu tunadhani linalenga kuchelewesha shauri hili," ameeleza Akyoo

Baada ya mvutano wa pande mbili kesi hiyo ikaahirishwa kwa dakika 15, ambapo baada ya kurejea Hakimu Mkazi Mwandamizi, Clescensia Mushi amesoma uamuzi mdogo uliyotokana na mawasilisho ya pande hizo.

Katika maamuzi hayo, Hakimu Clescensia ametupilia mbali maombi ya utetezi kwa madai kuwa mahakama itabeba jukumu la kukitafuta na kukipitia maelezo ya onyo ya mshtakiwa namba moja yaliyopokelewa mahakamani katika kesi ya jinai namba 10/2022 ili kulinganisha saini za mshtakiwa huyo.

"Nimepitia hoja za pande zote mbili lakini mahakama imejiridhisha kwamba hakuna sababu za msingi za kutoendelea na usikilizaji wa ushahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa. Kwa hiyo mahakama inatupilia mbali maombi ya uoande wa utetezi kwa sababu hoja zao hazina mashiko" ameeleza Clescensia

Hata hivyo, kabla ya kuendelea na ushahidi, wakili wa utetezi, Steven Kitale akasimama na kuieleza mahakama kuwa hawataendelea na kesi hiyo, kwani mshtakiwa namba 38, Mariam Julius ameugua ghafla na kupelekwa hospitalini.

Baada hoja hiyo, upande wa Jamhuri ukaiomba mahakama kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na wakili Kitale kwa madai kwamba mbinu hiyo inatumiwa na washtakiwa kuchelewesha shauri hilo.

Kwa upande wake, Hakimu Clescensia amekubaliana na maombi ya upande wa utetezi na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano Septemba 21, 2022 Saa 3:30 asubuhi itakapoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa utetezi.

Katika kesi ya msingi ya Jinai namba 12/2022 Zumaridi na wenzake 83 wanakabiliwa na shtaka la kufanya kusanyiko lisilo halali huku katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa kukiwa na mvutano wa uhalali wa saini katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa namba moja.