Mapya ajali ya Precision washirika wa Majaliwa wakiibuka

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Ziwa Victoria Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 ikitolewa kwenye maji.
Muktasari:
- Ni vijana waliowezesha abiria 24 ajali ya ndege kuokolewa
Bukoba/Dodoma. Jina la Majaliwa Jackson limekuwa maarufu ndani na nje ya nchi baada ya kijana huyo kuwezesha abiria 24 waliokuwa ndani ya ndege iliyopata ajali mjini Bukoba kuokolewa. Sifa na pongezi kwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, mchuuzi wa dagaa katika mwalo wa Nyamkazi ulioko jirani na Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Kagera zinatokana ujasiri na moyo wa kujitolea uliofanikisha kazi ya uokoaji baada ya kufungua mlango wa dharura wa ndege iliyoanguka katika Ziwa Victoria Novemba 6, mwaka huu.
Ndege ya Precision Air, 5H-PWF, ATR 42-500 ilianguka baada ya kushindwa kutua uwanjani hapo kutokana na hali mbaya ya hewa.
Wengi, wakiwemo viongozi wa Serikali wanammiminia sifa Majaliwa pekee kwa ujasiri na moyo wa kujitolea; lakini imebainika kijana huyo aliyezawadiwa fedha na ajira jeshini alishirikiana na wenzake watatu kuwezesha abiria hao kuokolewa kwenye tukio hilo.
“Tulikuwa vijana wanne wakati tunafanya jitihada za kutafuta namna ya kuwaokoa abiria wa ndege waliokuwa wakitupungia mikono kuomba msaada; pamoja na Majaliwa ambaye ndiye sifa zake zimevuma, nilikuwepo pia mimi Sadama Sadath, Ally Athuman na Jost Festo,” alisema kijana Sadama, mvuvi katika mwalo wa Nyamkazi Manispaa ya Bukoba.
Akizungumza na Mwananchi wakati wa mahojiano maalum eneo la Nyamkazi juzi, Sadath alisema kilichompatia sifa mwenzao hadi kutambulika ndani na nje ya nchi ni kitendo cha kuzimia baada ya mlango wa ndege uliofunguka ghafla na kwa kasi kumbamiza usoni hadi kuzimia na kulazwa hospitalini sawa na abiria waliookolewa katika ndege.
“Tulikuwa wote hapa mwaloni tukiendelea na shughuli zetu za kawaida wakati tunashuhudia ndege inakuja usawa wa eneo letu kabla ya kukata kona kurudi usawa wa bandari na uwanja wa ndege kabla ya kutua majini,” alisema Sadath.
Alisema baada ya kuona tukio hilo, yeye na wenzake walichukua mtumbwi kwa haraka na kuanza safari kwenda eneo la ajali, huku Majaliwa akiwa ameketi eneo la mbele la mtumbwi.
“Majaliwa alikuwa mbele ya mtumbwi, ikabidi tumpe kasia ili kuubamiza mlango wa dharura tulioelekezwa na rubani huku tukitumia kimkanda kuuvuta. Mlango ulifunguka ghafla kwa kasi na kumbamiza mwenzetu juu ya jicho hadi akazimia na kukimbizwa hospitalini pamoja na abiria waliookolewa kutoka ndani ya ndege,” alisema Sadath.
Festo, mvuvi mwingine aliyeshirikiana na wenzake, akiwemo Majaliwa kuufungua mlango wa ndege aliiambia Mwananchi ujasiri na moyo wa kujitolea haikuwa akili wala uwezo binafsi, bali ni nguvu na kudra za Mwenyezi Mungu kupitia kwao.
“Kiukweli haikuwa akili wala nguvu zetu…ile ilikuwa ni kazi ya Mungu aliyeonyesha nguvu na uwezo wake kupitia mikono yetu,” alisema Festo.
Kijana mwingine, Ally Athuman Kiboko ambaye ni kati ya vijana wanne waliofika wa kwanza eneo la ajali, alisema iwapo wangekuwa na vifaa vya kuzamia, wangeokoa watu wengi zaidi ya 24 waliookolewa katika ajali hiyo kwa sababu hadi wanalazimika kutoka ndani ya ndege baada ya maji kuzidi kujaa, walikuwa wanasikia sauti za watu wakiomba msaada.
“Tukiwa ndani ya ndege tukiwaokoa abiria waliokuwa eneo linaloonekana hadi kuhisi watu waliokuwemo ndani ya ndege wameisha, tulisikia dalili za kuwepo watu wengine eneo la mbele ya ndege. Tulishindwa kubaki ndani ya ndege tukihofia maisha yetu kwa sababu maji yalianza kuongezeka,” alisema Kiboko.
Alisema wakati wanalazimika kutoka ndani ya ndege kuepuka kuzidiwa nguvu, tayari maji yalishajaa hadi kuwafikia usawa wa shingoni.
“Mwenzetu Sadath ndiye aliyetoka wa mwisho ndani ya ndege maji yakiwa yanamfikia shingoni na muda mfupi askari kutoka vyombo mbalimbali walifika na kuwataka watu wote waliokuwa eneo la ajali wakiwemo wao kuondoka karibu na ilipokuwa ndege kwa tahadhari na usalama wao.
“Muda huo mwenzetu Majaliwa alishakimbizwa hospitalini kuokoa maisha yake kwa sababu alizimia baada ya mlango kufyatuka na kumgonga usoni,” alisema Kiboko.
Ombi la mafunzo, vifaa
“Tunaishukuru Serikali kwa uamuzi wa kumzawadia na kumpa ajira Majaliwa; lakini tunadhani muda umefika kwa vijana tunaofanya shughuli zetu ziwani kila siku tupewe mafunzo maalumu, ikiwemo ya kuzamia ili tuweze kutoa huduma za uokoaji pindi ajali zinapotokea jirani na maeneo tunayofanyia kazi,” alisema.
Pamoja na mafunzo kwa wavuvi na watu wengine ambao shughuli zao za kila siku hufanyika ndani ya maji, kijana huyo alishauri Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Mwaloni (BMU) vikabidhiwe vifaa vya uokozi, vikiwemo mavazi maalumu ya kuzamia na mitungi ya hewa kwa vijana watakaopewa mafunzo ya kuzamia.
“Uzoefu unaotokana na matukio ya ajali za maji nchini unaonyesha vijana wavuvi katika maeneo ya ajali au yaliyo karibu ndio huwa wa kwanza kufika na kutoa msaada; kutuwezesha ni njia muhimu katika kupunguza madhara, ikiwemo vifo vya ajali za majini kama ilivyo kwa ajali ya ndege (ya Bukoba),” alisema mvuvi huyo kijana.
Alisema japo ni gharama kununua boti za mwendo kasi na vifaa vya uokozi, ni gharama zaidi kupoteza maisha hata ya Mtanzania mmoja kwa kukosa msaada wa haraka wakati wa dharura ya ajali.
“Tupatiwe mafunzo na ujuzi wa kuzamia na kuwezeshwa vifaa ili ujuzi wetu utumike kuokoa maisha ya Watanzania wakati wa majanga hasa ya majini,” aliongeza.
Majaliwa atinga mjengoni
Juzi, Majaliwa alifika bungeni jijini Dodoma na kukaa jukwaa la wageni wa Spika, akiwa amevalia suti nyeusi akiwa nadhifu huku akipongezwa kwa ujasiri wake kwa kushirikiana na wengine kufanya uokoaji.
Majaliwa aliongozana na askari kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Shaban Mkingilo na Mchungaji Peter Barnaba.
Akitoa pongeza kwa niaba ya Bunge, Spika Tulia Ackson alisema Majaliwa alifanya kwa kazi nzuri na kwamba japokuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, ni lazima Bunge litambue juhudi zilizofanywa na kijana huyo.
“Lakini nafahamu amekuja hapa kwa niaba ya kundi kubwa la wavuvi ambao walishiriki katika zoezi la kuwaokoa abiria na kusaidia kutoa miili ya marehemu ambao hawakubahatika,” alisema Spika Tulia.
Aidha, alimpongeza mama wa Majaliwa kwa kumlea kijana wake katika hali ya kumpa ujasiri wa kujiamini na kwamba amefanya jambo zuri pamoja na mazingira aliyonayo.
Hata hivyo, baadaye alisimama Mbunge wa Mkalama (CCM), Francis Mtinga na kuomba mwongozo wa kumpongeza pia baba mzazi na Spika Tulia alimtaka mbunge huyo kumpongeza yeye.
Hatua hiyo ilimfanya mbunge huyo kuanza kumpongeza baba huyo ambapo alisema anampongeza kwa niaba ya wabunge na Bunge zima.
Kauli hiyo ilimfanya Spika kumkatisha na kusema anayeruhusiwa kupongeza kwa niaba ya Bunge ni Spika, wajibu ambao alishaufanya kwa kumpongeza Majaliwa na mama yake aliyemlea.
Hatua hiyo, ilimfanya Mtinga kumpongeza baba yake Majaliwa kwa malezi mazuri ambayo amemlea na kumfanya kuwa shupavu sana. Baada ya hapo Dk Tulia alisema amempongeza mama yake kwa sababu maalumu na habari ya baba ameshampongeza Mtinga.
Naye, Dk Hamis Kigwangalla (Nzega-CCM) aliomba mwongozo akitaka wabunge wote wachangie Sh50,000 kutoka katika posho zao za jana ili kuonyesha ishara ya kutambua mchango wa Majaliwa.
Hata hivyo, Dk Tulia alisema kanuni aliyoitumia ilikuwa kinyume cha uhalisia kisha akasema: “Wote mmemuona, wahudumu wakati waziri mkuu akizungumza, mtapita, mtakusanya michango yenu ya kumpongeza na litakuwa jambo la heri.”