Marekebisho sheria za uchaguzi yatua bungeni

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Muktasari:

  • Baada ya Serikali kuahidi kuwasilisha marekebisho ya sheria za uchaguzi kwa makundi mbalimbali, leo imewasilisha miswada mitatu kuanza mchakato wa marekebisho sheria hizo.

Dodoma. Mchakato wa marekebisho ya sheria za uchaguzi umeanza bungeni ambapo leo Novemba 10, 2023, Serikali imewasilisha bungeni kwa mara ya kwanza miswada miwili.

Miswada hiyo ni pamoja na wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria  za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.

Mbali na miswada hiyo inayohusu uchaguzi, pia miswada miwili iliwasilishwa kwa mara ya kwanza ya Sheria ya Uwekezaji wa Umma wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2023.

Akizungumza bungeni Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema miswada hiyo mitano itapelekwa katika kamati mbalimbali za Bunge ikiwemo ya Utawala, Katiba na Sheria, Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na nyingine pengine Tamisemi.

 “Miswada hii ishasomwa kwa mara ya kwanza na sasa nitaelekeza katika kamati husika muda utakapofika,” amesema Dk Tulia.

Kupelekwa kwa miswada hiyo, kunatimiza ahadi ya Serikali ya kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi mara baada ya makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kutoa mapendekezo yao kuhusu sheria hizo.

Novemba 6, 2023, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25, amesema Serikali inakadiria kutumia Sh47.42 trilioni katika mwaka 2024/25.

Alisema shughuli za chaguzi za Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025 zikizingatiwa.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika mwakani ukifuatiwa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.